WALIOFARIKI KWENYE KIVUKO WAFIKIA 86...CHANZO CHATAJWA


Saa zaidi ya 20 tangu kuzama kivuko cha MV Nyerere, idadi ya watu waliokufa imefikia 86.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella hadi leo saa 4 na dakika 44 asubuhi Septemba 21, 2018 jumla ya maiti 86 zimeopolewa ambapo miili 42 imepatikana leo asubuhi, wakati mingine 44 ilipatikana jana.

“Watu 40 wameokolewa wakiwa hai, bado tunaendelea na zoezi la uokoaji”, amesema Mongella.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cornel Maghembe amesema kuwa sababu ya kuzama kwa kivuko hicho inasadikika kuwa ilibeba watu zaidi ya 400 ambapo kilizidisha uwezo wake ambao ni watu 101.

Maghembe amesema kuwa imezama mita chache kabla ya kuwasili eneo la Ukara ambapo dereva alipunguza mwendo kuashiria amekaribia kutia nanga ndipo abiria wengi walihamia upande wa lango la kutokea wakiwahi kusogea ili washuke ndipo uzito ulizidi na kupinduka.

“Abiria walipoona mwendo umepunguzwa walikimbilia kuwahi mbele ya lango ili kujiandaa kushuka, ndipo uzito ukaegemea upande mmoja”, amesema Maghembe.


Baada ya kusitishwa kwa zoezi la uokoaji wa abiria wa ajali ya kivuko cha MV. Nyerere jana jioni baada ya giza kuingia, limeendelea leo alfajiri ambapo hadi sasa waokoaji waliozama majini bado hawajatoka.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi Jonathan Shana, amesema kuwa tayari kikosi cha uokoaji kimeshaanza uokoaji tangu saa 11 alfajiri ambapo hadi walipositisha zoezi hilo tayari walikuwa wameopoa miili 44 na waliohai 32.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527