HATMA YA NONDO KUJULIKANA OKTOBA 2

Mahakama ya Hakimu Mfawidhi mkoa wa Iringa imefunga kusikiliza ushahidi wa shauri linalomkabili mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi Abdul Nondo baada ya kusikiliza mashahidi wawili wa upande wa utetezi, ambapo imepanga Oktoba 2 kutaja siku ya kutoa hukumu ya kesi hiyo.


Kabla ya kufunga ushahidi huo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya mkoa Iringa Liad Chamshama amesikiliza mashahidi wawili wa upande wa utetezi ambapo shahidi wa kwanza ni Abdul Nondo na shahidi wa pili ni Alphonce Lusako.


Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu jana Abdul Nondo akiongozwa na wakili wake Jebra Kambole, Nondo amedai kuwa alitekwa na watu wasiojulikana karibu na geti la chuo cha maji ubungo majira ya saa tano Usiku, siku ya tarehe 6 Machi 2018, kwa kuvamiwa na kutupwa siti ya nyuma ndani ya gari.


Nondo amesema watu hao walikuwa wakimhoji kwanini anatumiwa na wanasiasa kiasi cha kuvuruga amani na walimtuhumu kuwa anatumiwa na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Zitto Kabwe na Hellen Kijo Bisimba (aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu-LHRC) pamoja na kumshutumu kuwa yeye ni wakala wa Mange Kimambi katika kuandaa maandamano ya wanafunzi lakini amekana tuhuma hizo.


Kwa upande wake shahidi wa pili Alphoce Lusako ambaye ni kiongozi mwezake katika shirika la TSNP ameiambia mahakama kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa Paul Kinabo kuwa amepokea ujumbe kwa njia ya simu kutoka kwa Nondo kuwa yupo hatarini na ndipo wakatoa taarifa kwa uongozi wa chuo na askari wasaidizi wa chuo na kupewa RB.


Mtuhumiwa Abdul Nondo alifikishwa Mahakamani Machi 21, 2018 na kusomewa mashitaka yake ambayo yote aliyakana kuhusika nayo hivyo Oktoba 2 mwaka huu Mahakama itarejea tena kwa ajili ya kutaja siku ya hukumu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527