GUMZO LA MGONJWA ALIYEKUTWA NA KIJIKO,VITAMBAA NA BETRI YA RADIO TUMBONI KAGERA



Hospitali Teule ya Wilaya ya Missenye ya Mugana mkoani Kagera imefanya upasuaji na kutoa kijiko, betri ndogo ya redio na vitambaa kwenye tumbo la mgonjwa wa akili.

Vitu vingine vilivyotolewa vilivyokuwa vimeziba njia ya haja kubwa na kumfanya apate maumivu makali ya tumbo ni vibiriti viwili vya gesi, mswaki na ganda la limao.

Dk Eliud Nyonyi aliyeshiriki kumfanyia upasuaji mgonjwa huyo amesema baada ya vitu hivyo kutolewa hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri.

“Hiyo picha inayosambaa mitandaoni sijaiona, lakini ni kweli kuna mgonjwa tumemfanyia upasuaji na tumemkuta hivyo vitu tumboni, ila siwezi kuzungumzia zaidi taarifa za mgonjwa,” alisema.

Picha inayoonyesha vitu hivyo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao mbalimbali huku kila mtu akisema lake kuhusu vitu hivyo.

Dk Nyonyi ambaye anakaimu nafasi ya mganga mkuu wa hospitali hiyo alimtaja mgonjwa huyo kuwa ni Eliud Novart (25) na kwamba, bado amelazwa katika wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji akiendelea kupatiwa matibabu.

Akizungumzia tukio hilo, mganga mkuu wa Wilaya ya Missenye, Dk Hamis Abdallah alisema Novart alifikishwa katika Hospitali ya Mugana baada ya kupatiwa rufaa na Hospitali ya Nyakahanga iliyopo wilayani Karagwe akitokea Kyerwa.

Hata hivyo, Dk Abdallah alisema mgonjwa huyo alipofanyiwa kipimo cha x-ray alionekana kuwa na vitu ndani ya tumbo, ndipo Agosti 28 madaktari walipoamua kumfanyia upasuaji.

“Huyu mgonjwa baada ya upasuaji alikutwa na kijiko, vibiriti vya gesi, betri ndogo na ganda la limao na matibabu yake ni changamoto kwa kuwa mtu mwenyewe ni mgonjwa wa akili, kuna wakati anagoma kunywa dawa au kuchomwa sindano,” alisema Dk Abdallah na kuongeza kuwa kama angecheleweshwa kufikishwa hospitali kulikuwa na hatari ya utumbo kupasuka.

Alisema kwa mwonekano, vitu hivyo vinakadiriwa kukaa tumboni kwa takriban saa 48.

Mganga huyo wa wilaya alishauri wagonjwa wenye matatizo ya akili kupatiwa uangalizi wa kutosha na wasitengwe.

Hata hivyo aliwashauri ndugu kutokaa nao nyumbani, bali wawapeleke hospitalini ambako kuna kitengo cha kutoa ushauri kwa wagonjwa wa aina hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527