Thursday, August 16, 2018

WAZIRI MKUU AAGIZA KUKOMESHWA VITENDO VYA UBAMBIKIZAJI KESI WANANCHI

  Malunde       Thursday, August 16, 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza ofisi za masuala ya sheria kuhakikisha kuwa vitendo vya ubambikizaji wa kesi vinakoma na mashauri yanayofikishwa mahakamani yanakuwa na ushahidi wa kutosha.


Akizungumza jana katika uzinduzi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, alisema ni matarajio ya Serikali kila moja ya ofisi hizo sasa itapanua zaidi wigo wa utendaji wake hadi kufikia ngazi ya wilaya.


“Ofisi ya hizi zinategemewa kuwa mkono wa Serikali katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ubambikazaji wa kesi vinakoma na kuhakikisha kuwa kesi zinazofikishwa mahakamani zina ushahidi wa kutosha,” alisema Majaliwa.


Alisema malengo makubwa ni kuufanya umma kuelewa vizuri masuala ya kisheria na utoaji haki ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko yenye tija kwa sheria.


“Na mabadiliko hayo yaanze kwanza na sheria zetu kusomeka kwa lugha ya Taifa, lakini pili uendeshaji wa kesi nao uangaliwe, utoaji hukumu nao uangaliwe na hata hati za hukumu zisomeke kwa lugha ya Kiswahili ili watu wa kawaida waweze kuwa na uelewa mpana katika suala hili,” alisema.


Wakili wa kujitegemea mkoani hapa, Elias Machibya alisema kesi za jinai angalau zina mwongozo ambao una kanuni zake.


Machibya alisema kesi ikifunguliwa na upelelezi ukawa haujakamilika ndani ya siku 60, mahakama inakuwa na mamlaka ya kuifuta.


“Kuna kesi kubwa ambazo haziangukii katika hilo fungu maana yake ni kwamba mtu anaweza kupelekwa mahakamani na ushahidi haujakamilika,” alisema. “Kuna kesi inayokwenda hadi kusikilizwa, lakini bado upelelezi haujakamilika, (waendesha mashtaka) hawana ushahidi wa kutosha na (washtakiwa) wamekuwa wakiachiwa, wengine wamekuwa wakikata rufaa mahakama za rufaa zinawaachia.”


Wakili huyo alisema kuwa hilo huathiri kwa kiasi kikubwa wananchi kwa sababu makosa mengine hayana dhamana na wananyimwa uhuru wao.


“Serikali inapaswa kuimarisha vitengo vya upelelezi na kanuni za kupeleleza makosa zifuatwe, wanaohusika na upelelezi wapewe mafunzo na vifaa,” alisema Machibya.


Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema wizara yake inaandaa muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali na wanapendekeza kuifanyia marekebisho sheria ya utekelezaji wa majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG) Sura ya 268.


Alisema marekebisho hayo yanalenga kumpa mamlaka AG, kutoa maelekezo ya jumla na mahsusi kwa wanasheria walioko kwenye utumishi wa umma wa jinsi ya kutekeleza majukumu yao katika maeneo yao ya kazi.


“Tunaamini kwa kufanya hivi wanasheria walioko kwenye utumishi wa umma watatekeleza kazi zao vizuri bila kuiingiza Serikali katika migogoro,” alisema.


Akizungumzia uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema ofisi hizo zinakamilisha uwepo wa mihimili yote mitatu mjini Dodoma.


“Mahakama Kuu imetengewa eka 50 na ofisi za mabalozi zimetengewa eka 1,800; na wanatakiwa kuanza ujenzi mara moja,” alisema.


Akizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Majaliwa alisema ni matarajio ya kila mwananchi kuwa itapanua zaidi wigo wa utendaji hadi ngazi ya wilaya. “Ofisi hii inategemewa kuwa mkono wa Serikali katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ubambikizaji wa kesi vinakoma na kuhakikisha kuwa kesi zinazofikishwa mahakamani zina ushahidi wa kutosha,” alisisitiza.


Kuhusu ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, alisema ndiyo mtetezi na mlinzi namba moja wa haki za Serikali.
Na Rachel Chibwete, Mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post