WANAKIJIJI DIDIA WATAPELIWA UMEME NA MAAFISA FEKI WA TANESCO

Baadhi ya wakazi wa kijiji na kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamejikuta wakifanyiwa utapeli wa fedha na watu wawili wasiowafahamu kwa ajili ya kuvuta nishati ya umeme vijijini (REA) kiasi cha shilingi milioni 5.


Inaelezwa kuwa watu hao walipiga simu kwa mwenyekiti wa kijiji hicho Chale Yoyo Chenye wakazi zaidi ya 4,000 na vitongoji tisa wakijitambulisha kuwa ni maafisa wa TANESCO ambapo mmoja akidai ni Meneja Msaidizi kutoka shirika la umeme nchini (TANESCO) na mmoja ni mkandarasi kutoka shirika hilo.

Akiongea na wandishi wa habari juzi mwenyekiti wa kijiji hicho Chale Yoyo alisema alipigiwa simu na watu ambao baada ya kujitambulisha walimtaka awaeleze wananchi kuhusu ujio wa umeme ndipo naye akatii agizo hilo kwa kuitisha mkutano wa hadhara.

Yoyo alisema wamejikuta wakifanyiwa utapeli wa fedha na watu wawili wasiowafahamu waliodai wanakuja kuvuta nishati ya umeme vijijini (REA) kijijini hapo hivyo kila kaya ichangie kiasi cha shilingi 37,000/=.

“Baada ya kuwaeleza wananchi kuhusu habari njema ya umeme waliitikia kwa wingi na kufanikiwa kukusanya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni (5) tano”,aliongeza.

“Nilipowahoji kwanini tunatakiwa kutoa kiasi hicho cha fedha badala ya shilingi 27,000/= kama serikali inavyotangaza walidai nguzo ni chach, hivyo kila mmoja atoe shilingi 37,000/= kwani shilingi 10,000 kwa ajili ya Main switch na kusisitiza kuwa wakikamilisha kuchanga ndipo watawapatia akaunti namba ya benki waziweke humo hizo pesa”,alifafanua Yoyo.

Hata hivyo mwenyekiti Yoyo alieleza kuwa baada yakukusanya zaidi ya shilingi milion tano kwa baadhi ya wananchi ndipo aliwapigia simu watu hao ili watume namba ya akaunti ya namba ya benki ,wakatuma akaunti namba ya mtu binafsi ambapo alishtuka na kuwaomba tena akaunti ya TANESCO.

Yoyo alisema baada ya kuhisi kuwepo udanganyifu aliamua kumtafuta Meneja wa TANESCO mkoa wa Shinyanga kupata ufafanuzi zaidi juu ya suala hilo ndipo alipomjibu kuwa watu hao ni matapeli asithubutu kutoa fedha hizo kwani zoezi la uwekaji nishati hiyo huko bado halijafikiwa.

Kufuatia hali hiyo,Mwenyekiti wa kijiji aliamua kurudisha fedha kwa wananchi.

Baadhi ya Wakazi wa kitongoji cha Danduu , Amos Shija na Fatuma Hussein waliochangishwa fedha kiasi cha shilingi 37,000 na kupatikana kiasi cha shilingi million tatu katika mtaa huo walisema baada kuwaelezwa kwenye mkutano wa hadhara juu ya ujio wa umeme watu walishangilia sababu walikuwa na uhitaji wa muda mrefu lakini baada kuambiwa kuwa ulikuwa ni utapeli wakarudishiwa fedha zao.

Diwani wa kata ya Didia Masele Luhende alisema taarifa hiyo aliipata kutoka kwa mwenyekiti wa kijiji hicho namna alivyotaka kutapeliwa fedha kwa kuwachangisha wananchi ambapo alimtaka kuwa makini na matapeli.

Ofisa uhusiano wa shirika la umeme (TANESCO ) mkoani Shinyanga Sarah Libogoma alisema uwekaji wa nishati ya umeme una utaratibu wake kwa kushirikisha viongozi wa vijiji,kata na wananchi watu hao wameamua kutumia vyeo vya shirika hilo ili waweze kuaminika.

Alisema shirika hilo lina taratibu zake za kuwasiliana na wananchi kuhusu namna ya kuwapatia nishati ya umeme na utaratibu huo unafahamika vizuri siyo kwa njia ya simu.

Na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527