WABUNGE MBARONI KWA KUSHAMBULIA GARI LA RAIS

Baadhi ya wabunge nchini Uganda wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kushambulia gari la Rais Yoweri Museveni kwenye uchaguzi mdogo eneo la Arua.

Jeshi la polisi limeeleza kuwa linawashikilia watu 30 ikiwa ni pamoja na wabunge kutoka Kampala, Njiri na maeneo mengine ambao wanadaiwa kuhusika kwenye tukio hilo lililotokea jana na kusababisha kifo cha mlinzi wa mbunge aliyeuawa kwa kufyatuliwa risasi na askari polisi.


“Hadi tunavyoongea hivi sasa hao wote tunawashikilia kwenye selo zetu, hatujui kama kati ya hao kuna waandishi wa habari au la. Tukianza kuwachambua tutafahamu ukweli wa jambo hili,” msemaji wa polisi wa eneo la West Nile, Josephine Angucia aliiambia NTV.


Aliongeza kuwa watu hao waliokamatwa walikuwa kwenye kundi ambalo lilirusha mawe kupiga gari linalotangulia msafara wa Rais.


Akizungumzia kifo cha mlinzi wa mbunge, alisema kuwa kifo chake kilitokana na risasi iliyopigwa bila kumkusudia.


Rais Museveni alikuwa katika eneo hilo akimpigia kampeni mgombea wa chama chake cha National Resistance Movement, Nusura Tiperu.

Mbunge wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine alikuwa eneo hilo la Arua pia akimpigia kampeni mgombea binafsi, Kassiano Wadri. Mbunge huyo ni miongoni mwa wanaoshikiliwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527