THRDC : WANA HABARI WAMEJAWA NA HOFU KUBWA YA KUTOA TAARIFA WANAZOHISI HAZITAFURAHISHA WATAWALA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umesema matukio ya kupigwa na kuteswa kwa raia wakiwa mikononi mwa polisi yanaongezeka siku hadi siku na kuongeza hofu kwa jamii juu ya uwapo wa utawala wa sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema matukio hayo yanaongezeka huku baadhi ya watu wakitishwa na kuambiwa siyo raia na wengine kunyang'anywa pasi za kusafiria.

Alisema wanalaani vikali vitendo vya karibuni vya ukiukwaji wa sheria na haki za waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu kunakofanywa na Jeshi la Polisi lenye wajibu wa ulinzi wa raia na mali zao.

"Tunashuhudia waandishi wakipigwa na kukamatwa na polisi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi," alisema.

Alisema kuwa Agosti 8, mwaka huu, mwandishi wa habari wa Wapo Radio, Silas Mbise, alishambuliwa na kukamatwa na polisi akiwa kazini na alipigwa waziwazi na polisi wenye silaha huku akiwa amelala chini na hana silaha yoyote.

Alisema kuwa tukio lingine la hivi karibuni ni la mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma, aliyepigwa na kukamatwa na maofisa wa polisi wakati akichukua habari katika mkutao wa kampeni za uchaguzi wa diwani wilayani Tarime mkoani Mara.

"THRDC ilitoa msaada wa kisheria ili kumwezesha kupata dhamana na wakili wake Ernest Muhagama alisema alipofika polisi alielezwa kwa mtuhumiwa huyo kakamatwa kwa kosa la kuandamana kinyume cha sheria. Aliachiwa kwa dhamana Agosti 9," alisema.

Aliyataja matukio mengine ni ya miezi miwili iliyopita dhidi ya wa waandishi wa habari kuwa ni yaliyofanywa dhidi ya George Ramadhani na Christopher Gamaina, waliokamatwa na polisi mkoani Mwanza wakati wakiwa wanatekeleza majukumu yao na walifunguliwa mashtaka mahakamani.

Alisema mwandishi mwingine ni Emmanuel Kibiki aliyekamatwa na polisi mkoani Iringa na kulazimishwa kulala polisi kwa siku kadhaa kabla ya kufikishwa mahakamani.

"Kwa ujumla, hali ya uhuru wa wanahabari na vyombo vya kawaida na vya mitandaoni umezidi kutoweka na kupelekea kuzuia Watanzania kupata habari sahihi na kwa wakati kwa mujibu wa Katiba," alisema.

'Kwa sasa, wanahabari wamejawa na hofu kubwa kutoa taarifa zozote watakazohisi hazitawafurahisha baadhi ya watawala," alisema.

"Tunasikitishwa na kuongezeka kwa matukio ya kupigwa na kukamatwa kwa wanahabari bila sababu za msingi na za kisheria. Wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na polisi," alisema.

Kwa mujibu wa Olengurumwa, polisi ni chombo muhimu kinachotakiwa kusimamia uhuru na usalama wa waandishi wa habari na siyo kuwashambulia kama ilivyotokea mara kadhaa kwa baadhi ya maofisa wa polisi kutumia nguvu kubwa kuwashambulia na kuwajeruhi wanahabari wakiwa kazini.


"Ni lazima ikumbukwe kuwa kila mtu anayo haki ya ulinzi kwa mujibu wa sheria za nchi, vyombo vya dola vina wajibu wa kuwalinda raia na mali zao ikiwemo waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu Tanzania," alisema.


Aliongeza kuwa matukio ya watu kuhojiwa uraia wao yanazidi kuongezeka na sasa wamefika viongozi na raia saba wanaodaiwa siyo raia licha ya kuzaliwa na kuishi Tanzania kwa maisha yao yote.


Aliwataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Askofu wa Jimbo la Ngara, Severine Niwemugizi, Olengurumwa, Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, Abdul Nondo, Mkurugenzi wa Twaweza na Aidan Eyakuze.


Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), Maanda Ngoitiko na Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe.


"Matukio kama haya yakiendelea kutokea hasa dhidi ya watetezi wa haki za binadamu, yataendelea kusababisha hofu na kupoteza uhuru wa watetezi wa kufanya kazi zao kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi," alisema na kuongeza:


"Matumizi ya nguvu kupita kiasi na kutojali utawala wa sheria pia vimezidi kuchangia kuzorota kwa hali ya watetezi wa haki za binadamu nchini.


"Baadhi ya vyombo vya dola vinatumia nguvu kubwa kuingilia uhuru wa asasi za kiraia na watetezi wanapotaka kufanya mikutano ya ndani na kudai kuwa lazima wawe na vibali au hali ya usalama hairuhusu mikutano hadi ya ndani."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527