SERIKALI YATANGAZA AJIRA 1500


Serikali inatarajia kutoa ajira 1,500 kwa askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji kwa mwaka wa fedha 2018/19, ili kuondoa tatizo linalolikabili pamoja na kutenga zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa jeshi hilo ili liweze kutoa huduma zitakazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza jana Agosti 29, 2018 katika wiki ya Jeshi la Zimamoto katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alisema ajira hizo zitaongeza kasi ya kukabiliana na majanga ya moto yanayojitokeza maeneo mbalimbali nchini.

“Tunatambua changamoto ya upungufu wa wafanyakazi katika kikosi hiki hivyo tutaajiri watumishi 1,500 ili kuongeza nguvu iliyopo,” alisema Lugola.

Katika hatua nyingine, Lugola amewaagiza wakurugenzi wote wa majiji pamoja na miji kutoruhusu ujenzi holela na badala yake wazingatie mipango miji kwa sababu unasababisha vikosi vya zimamoto kushindwa kufika eneo la tukio kwa wakati.

Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, Thobias Andengenye alisema wanakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi ikilinganishwa na ukubwa wa nchi na idadi ya wananchi na kutaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa magari katika ofisi za mikoa na wilaya na kupendekeza magari 100 yatasaidia kufanya kazi kwa urahisi.

Agosti 19 magari saba ya mizigo yaliteketea kwa moto katika kituo cha forodha Rusumo wilaya ya Ngara, mpakani mwa Tanzania na Rwanda, baada ya gari moja la mafuta ya petroli kuligonga gari jingine hali iliyopelekea Helkopta ya jeshi la Rwanda kusaidia kuzima moto ulioteketeza shehena iliyokuwa imepakiwa na magari hayo baada ya kukosekana kwa magari ya zimamoto wilayani humo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post