MAAJABU YA CHEMCHEMI YA MAJI MOTO YA 'MTEMI MALEMBELA' SHINYANGA


Na Kareny Masasy - Shinyanga

KILOMITA 16 kutoka Shinyanga mjini ukiwa unaelekea jijini Mwanza, ndipo kilipo Kijiji cha Ikulilo chenye Kitongoji cha Uzogore inapopatikana chemchemi ya maji moto. 

Hapa ndipo kuna maajabu ambayo pia, ni kivutio kikubwa cha utalii ambacho ama kwa kutoeleweka kutokana na kutotangazwa vizuri, huenda hakijajulikana na kutumika ipasavyo.

Hapana shaka kwamba, katika maeneo mbalimbali watu wanapotafuta maji ya baridi nje ya maeneo ya kazi au nyumbani, mara nyingi hutafuta kilipo kisima. Hii inatokana na ukweli kuwa, mara nyingi visima huwa na maji baridi. 

Katika Kitongoji cha Uzogore kijijini Ikulilo, Kata ya Ibadakuli katika Manispaa ya Shinyanga, hali ni tofauti kabisa. Hapo ipo chemchemi ya ajabu inayotoa maji ya moto mithili ya yanayochemshwa jikoni.

 Inaelezwa kuwa, hili ni eneo lililokuwa makazi ya Mtemi wa Kabila la Wasukuma aliyefahamika kwa jina la Mtemi Malembela.

Inadaiwa kuwa, baada ya kifo cha Mtemi Malembela, alizikwa hapo na mpaka sasa, ibada za matambiko ya wanaukoo wa Malembela hufanyika hapo. 

Kimsingi, maji hayo yanapotoka ka tika chemchemi hiyo ardhini, huwa yanachemka na kutokota mithili ya yaliyo tayari kwa kusongwa ugali murua. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikulilo, Peter Dotto, maji hayo yaliyoshuhudiwa na mwandishi wa makala haya hivi karibuni yakichemka, yana ladha ya chumvi.

Dotto anasema: “Maji haya hutiririka kila wakati; hayana kipindi cha kiangazi wala masika na pia, hayajulikani chanzo chake ni kipi.” 

Anasema yanapotiririka husambaa na hata kuingia katika mto uliopo jirani uitwao Mto Mhumbu katika Manispaa ya Shinyanga.

 Anasema baadhi ya wanakijiji hutumia maji ya eneo hilo kwa kuoga, kufulia nguo na hata mahali hapo kuwa moja ya sehemu zao muhimu na maarufu kwa kutembelea na kupumzika. 

Licha ya kuyatumia kwa utalii wa mapumziko, Mwenyekiti huyo anasema maji hayo yamewasaidia baadhi ya wanawake kujiingizia kipato kinachotumika katika familia zao kwa kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kununua sare na mahitaji mengine ya wanafunzi na watoto wao wengine.

Monica Joshua wa kijiji hicho anasema maji ya chemchemi hiyo yanashika vizuri sabuni na kutoa povu jingi ingawa yana chumvi na kwamba, anaamini ladha yake ya chumvi huua vijidudu vilivyopo kwenye nguo kama vile chawa.

 Aidha anasema maji hayo yamewasaidia baadhi ya wanawake kupata kipato katika familia zao na kuwanunulia sare za shule wanafunzi. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, anasema uongozi wa kijiji na uongozi wa Manispaa unapaswa kushirikiana kuboresha eneo hilo ili liwe kivutio cha watu kutembelea kuona maji hayo yanavyokuwa ya moto kisha kupoa.

Mkazi wa Kitongoji cha Uzogore, Regina Mhoja anasema hugandisha maji hayo na kuyatumia kupata magadi anayoyauza kwa kuyatembeza mjini. 

Anasema kipande kimoja cha magadi yaliyoganda huuzwa kwa Sh 200. Kwa mujibu wa Mhoja, hutumia chombo aina ya chungu huchota mchanga na kuuchemsha jikoni kwa kuchanganya na maji ya kawaida. Anasema mvuke unaotoka katika uchemshwaji huo hutengewa chombo maalumu na baadaye hupoa mithili ya upikaji wa pombe ya kienyeji.

“Nikimaliza, ninayaacha kwa kuyafunika usiku mzima na mwisho huganda na kuwa jiwe ambalo tunaliita magadi ambalo wananchi hutumia kulainishia mboga za majani, na dawa za kienyeji mtu anapokohoa,” anasema Mhoja. 

Kwamba wateja wake wakubwa ni wakazi wa mjini ambao wakati mwingine huwauzia kwa bei ya jumla sokoni. “Kutengeneza magadi hayo hakuhitaji gharama kubwa; kikubwa tu, ni kufuata maji hayo, kuyachuja na kuyagandisha kwa siku chache hivi, na mwisho yakiganda, unayagawa kwa kiwango cha pesa unachotaka kuuzia,” anasema.

Mkazi mwingine wa kitongoji hicho, Madebele Shija, anasema chemchemi hiyo licha ya kuwasaidia wajasiriamali kuingiza kipato, pia huwasaidia wafugaji kunywesha mifugo wao, kwani kadiri yanavyoendelea kutiririka ardhini kutoka kwenye chemchemi, huzidi kupoa kiasi cha kunywewa na mifugo.

 “Maji haya yana ladha ya chumvi na yana magadi yanapobubujika kutoka ardhini, huwa yanachemka kiasi kwamba huwezi kuyagusa, lakini ukiweka kwenye chombo baada ya muda, yanapoa na kuwa maji ya kawaida ya mifugo kuweza kunywa na ujue chemchemi hiyo haina msimu wa kiangazi wala masika; muda wote hutiririka,”anasema Shija.

Mtaalamu wa miamba ambaye ni Mhandisi wa maji, Lucas Said anasema kutokea kwa chemchemi yenye kutoa maji ya chumvi inatokana na eneo hilo kuwa na miamba yenye chumvichumvi. 

Mhandisi Said anasema kitendo cha miamba hiyo kutoa kutoa maji ya moto ni matokeo ya kuwapo volkano ya moto ardhini katika eneo hilo hali inayofanya maji kuchemka.

 Mmoja wa ukoo huo wa Mtemi Malembela, Malale Kwisu, anasimulia historia yenye maajabu yaliyotokea katika kifo cha Mtemi Malembela yapata miaka 100 iliyopita. Anasema maajabu hayo ndiyo kisa kinachoaminika kwao kuwa chanzo kikuu cha kupatikana chemchemi hiyo ya maji ya moto.

Anasema Mtemi Malembela alikuwa akiishi katika kijiji hicho na eneo lililo na chemchemi lililokuwa ni sehemu ya shamba alilolilima likiwa tambarare, bila kuwepo kiashiria chochote cha kuwapo chemchemi. 

Kwisu anasema japo hakumbuki ni mwaka gani, lakini wakati akiwa mdogo, dada wa marehemu Mtemi Malembela aliyefahamika kwa jina Sia, aliolewa na Mtemi Ngiriti kutoka eneo la Mwantini lililopo Shinyanga Vijijini. 

Kwamba, dada huyo aliolewa kwa ng’ombe 60, lakini akashindwa kuvumilia maisha ya ndoa, hivyo akarudi kwa kaka yake (Mtemi Malembela) alikokuwa akiishi katika Kitongoji cha Uzogore.

 Inaelezwa kuwa, baada ya Sia kumueleza kaka yake, kaka huyo (Malembela) alimkingia kifua kwa kumwambia abaki nyumbani huku akikataa ng’ombe 60 zilizotolewa kama mahari zisirudishwe.

Kutokana na hali hiyo, Mtemi Ngiriti aliyekuwa pia wa kabila la Kisukuma, alichukia kitendo cha shemeji yake (Malembela) na mke wake (Sia), kuwa kitu kimoja na kung’ang’ania mifugo hiyo. 

Kwisu anasema Mtemi Ngiriti aliamua kwenda kutafuta nguvu kwa watemi wenzake na kukutana na Mtemi Kajala wa Usule aliyeogopeka kwa Wasukuma akitajwa kuwa shujaa kwa kila jambo, ikiwa ni pamoja na kupigana kwa kutumia mikuki na mishale. 

Kwisu anasema katika makutano yao, Mtemi Ngiriti alimweleza shujaa huyo (Mtemi Kajala) kuwa, Mtemi Malembela ameungana na dada yake kumsaliti huku hataki kurudisha ng’ombe alizotoa kama mahari ya kumuoa Sia.

Kajala akamshauri kukusanya wafuasi wake kwa wingi ili vita ianze. Wakaunganisha nguvu. 

Anaeleza kuwa vita kali ilianza, kwa watemi kwa watemi wa kabila moja kwa kumvamia Malembela katika eneo lake la malisho ya mifugo lililokuwa Kolandoto na kuanza kukusanya mifugo yote aliyokuwa nayo ikiwemo mbuzi na kondoo.

 Lengo la kuchukua mifugo hiyo ilikuwa wagawane. Mtemi Kajala wa Usule akachukua mbuzi na kondoo, na ng’ombe wote wakawa wanachukuliwa na mwenyewe (Mtemi Ngiriti). 

Malembela alipoona kundi kubwa la watu, naye akaanza kukusanya watu na mdogo wake Mhina, lakini wakazidiwa nguvu katika mapigano kisha kunyang’anywa mifugo wake wote.

Baada ya kushindwa nguvu, Malembela alichukuliwa na watemi hao huku akiwa amefungwa kamba mikono yote miwili. 

Akapelekwa eneo la Mwantini kuelekea Chibe penye jiwe kubwa. Wakamlaza hapo na mifugo yake.

 Inadaiwa kuwa, baada ya kufika hapo, watemi hao walichinja ng’ombe dume mweusi na kisha wakachukua supu yake katika kibuyu; wakaichanganya na dawa, kisha wakamnywesha Malembela; akafariki dunia. 

Mwili wa Malembela ulitolewa Mwantini na kupelekwa eneo la Ndembezi lilipochimbwa kaburi lake na kuzikwa huko. 

Inalezwa kuwa baada ya miaka miwili, eneo hilo likaanza kutoa maji kwa kutokeza chemchemi ya maji kwenye kilima.

Kwamba, maji hayo yalikuwa siyo ya moto kama yalivyo sasa. Kwisu anasema, baada ya sehemu alipozikwa kuanza kutoa chemchemi ya maji, mwili ulihamishwa.

 Kwa imani yao, Kwisu anaeleza kuwa baada ya kutoka maji sehemu hiyo ilidaiwa mwili wa Mtemi Malembela ulihamishiwa eneo la Ndembezi na kuupeleka kwenye shamba lake la Uzogore. Anasema: “Hapo kwenye kaburi, chemchemi yenye maajabu ya kutoa maji ya moto yanayochemka, ikatokea na kuendelea hadi sasa.”

Katika simulizi lake, Kwisu anasema siku moja mke wa Mtemi Malembela akiwa shambani maji mengi yakitiririka bila kuwepo na chanzo chochote cha maji. Kadhalika siku ya pili na ya tatu akayaona mambo hayohayo. 

Akaamua kuwaeleza nduguze kinachotokea shambani. Siku ya nne alikwenda tena shambani ambapo maji yalitoka kwa kasi huku yakiwa na tope. 

Yakamlowanisha mwili mzima na kumfanya akimbie kwenda nyumbani na kuacha kulima. Mke huyo alisimulia tena kwa ndugu na kuweka hofu kubwa. Usiku wa siku hiyo, mke huyo akasikia sauti ya Malembela (mume wake) ikimueleza asiogope, bali awaeleze ndugu wachinje ng’ombe mweusi katika eneo hilo kama matambiko ya kimila ndipo wakatekeleza hayo.

Anasema siku iliyofuata, maji yakaanza kutiririka kidogo kidogo na chemchemi ikaanza kwa kutoa maji ya moto yaliyotokota kama yamechemshwa jikoni mpaka hii leo maji hayo ladha yake ni ya chumvi (magadi) ambapo watu kutoka sehemu mbalimbali hutembelea hapo na kuoga.

 Mkazi na mzee wa muiaka mingi katika kijiji hicho, Sayi Nyerobi anasimulia alivyoanza kuona chemchemi hiyo na kuwa ya maji ya moto. Anasema ingawa hajasoma na hajui mwaka wake wa kuzaliwa, lakini anayo kumbukumbu na ufahamu wa kuwepo chemchemi hiyo.

 Anasema zama hapakuwapo kitu chochote cha kushangaza katika eneo hilo, lakini anashangaa kwa nini maji yanayotoka hapo ni ya moto na hayatumiki kunywa, bali kama magadi kulainisha mboga.
Chanzo - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527