DIWANI AJIONDOA CHADEMA AKIDAI ENEO LAKE LIMEZUNGUKWA NA VIONGOZI WA CCM

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Rungwe, Mbeya kimemfuta uanachama na kumvua udiwani, Diwani wake wa Kata ya Kambasegela, Kiswigo Mwakalebela kwa madai ya kukiuka taratibu na kanuni za chama hicho.

Hata hivyo, Mwakalebela mwenyewe amesema amejivua uanachama na kuhamia CCM kwa madai kuwa anashindwa kufanya kazi kwa kuwa amezungukwa na viongozi wengi wa CCM.

Mwenyekiti wa Chadema halmashauri ya Busokelo, Furaha Mwakalundwa ameliambia Mwananchi kwamba baada ya kujiridhisha kupitia intelijensia ya chama hicho kuhusiana na mwenendo wa Mwakalebela walibaini amekuwa akiivunja katiba ya Chadema hivyo hawawezi kumvumilia.

“Chama kina taratibu na falsafa zake na chama hiki ni kikubwa kuliko mtu na diwani anapatikana kwa misingi ya Chadema hivyo inapotokea mtu unavunja na kukiuka katiba ya chama, basi hatuna budi kumchukulia hatua na ndicho kilichotumika kwa huyu mwenzetu Mwakalebela,” amesema Mwakalundwa.

Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala hilo Mwakalebela amesema hana taarifa za kufukuzwa na chama chake bali ameamua kujivua uanachama na udiwani kwa hiyari yake baada ya kuona anashindwa kumudu kuwatumikia wananchi kutokana na kukosa ushirikiano na viongozi ngazi za vijiji na vitongoji.

“Mimi sijavuliwa wala kufukuzwa uanachama kwani sina ugomvi na viongozi wa Chadema. Ila dhamira yangu imenisuta kwani niliona nashindwa kuwatumikia wananchi kwa kukosa ushirikiano wa viongozi ngazi ya chini.

Amesema anapata wakati mgumu kufanya kazi kwani wenyeviti wanaomzunguka wa vijiji na vitongozi ni wa CCM, hivyo hata kuamuru kufanya jambo fulani anashindwa kupata nguvu ya pamoja.

Amesema anaamini kwamba ili kuwatumikia ipasavyo wananchi wa kata hiyo anapaswa kurudi CCM ili aungane na kundi ambalo ni kubwa na lenye uamuzi wa sauti moja bila kutifuana, hivyo ameamua kurudi CCM akiamini atagombea upya kupitia CCM na atarudi kuwatumikia wananchi.

“Tunapokuwa na jopo kubwa na la pamoja kunakuwa na nguvu. Hivyo nimeona nirudi CCM na nitagombea tena kwani kazi ni ile ile ya kuwaongoza wananchi huku nikiwa na kundi la watu wenye uamuzi wa pamoja katika kufanya jambo” amesema.

Halmashauri ya Busokelo ina kata 13 na kati ya hizo CCM inaongoza Kata 12 na moja ndio iliyokuwa inashikiliwa na Mwakalebela.

Na Godfrey Kahango, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527