KATIBU MKUU WA CCM AFUNGUKA KILICHOMFANYA "APANIKI" KWENYE MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI

Siku mbili baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, kufanya mkutano na waandishi wa habari na baadhi ya watu kudai kwamba sifa ya kuibua mijadala aliyonayo imeingia dosari kutokana na namna alivyojibu maswali ya wanahabari, mwanazuoni huyo ameibuka na kusema hajutii.



Katika mahojiano kwenye kipindi cha televisheni cha 360 kinachorushwa na Clouds Tv, Dk. Bashiru alisema alionyesha ukali na hajutii jambo hilo.


“Kuna yule (anataja chombo chake) alinikera kwa kuhoji elimu yangu, akisema kwamba sijaitumia vizuri kukidhi matarajio na kwamba mimejibu rojorojo, huko ni kuwatukana Watanzania ambao wamenisomesha.


“Anapohoji uwezo wangu kielimu anawahoji walionisomesha kwa vipesa vyao, kwa kuwa nimesoma katika shule za umma tangu mwanzo,” alisema.


Alisema yeye ni mwanataaluma ambaye hakuwahi kununua mtihani wala kushindwa popote, akiwa na maandiko yake ambayo mtu anaweza kuyakosoa, lakini yanakubalika ubora wake.


Dk. Bashiru alisema huenda sehemu ya maarifa hayo ndiyo yaliyompa nafasi aliyonayo sasa, kwahiyo si sahihi kuhoji rejareja kwa kuanza na swali linalokera.


Alisema Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alimpigia simu na kumweleza kuwa alipoulizwa swali hilo alipaswa kushuka badala ya kupanda na yeye akamjibu aliamua kupanda naye (mwandishi) na angepata nafasi angepanda naye zaidi.


“Lengo lilikuwa ni kutuma ujumbe kwamba wanapokusanyika kuzungumza, waheshimiane kwa sababu masuala ya mijadala yanahitaji kusikilizana,” alisema.


Alisema mijadala ni tofauti na porojo, kelele na mizaha katika mazungumzo, lakini mkutano wake na waandishi wa habari ulikuwa ni fursa muhimu kwao na yeye pia katika kuwasiliana na umma.


“Lakini mimi sikuridhika na naamini waandishi pia hawakuridhika,” alisema.


Kuhusu swali aliloulizwa kwamba kama CCM imeshindwa kuheshimu katiba yao ni vipi kitaheshimu ya nchi, alisema anamfahamu mwandishi aliyemuuliza swali hilo kuwa ni mwanachama wa Chama cha CUF na kwamba swali lake lilikuwa na mwelekeo wa kiitikadi.


“Hawa wanahabari walichukua mwelekeo wa kiitikadi na kuwakosesha watazamaji wasaa wa kupata ufafanuzi mzuri kwa namna swali linavyoundwa,” alisema.


Akizungumzia ustahimilivu wake kisiasa, Dk. Bashiru alisema anaweza kuvumilia jambo ambalo halimuui, lakini hawezi kuvumilia lile analoona linamuua na kwamba atakapoona anauawa atajitetea ili aendelee na mijadala.


Akizungumzia siasa za matusi, Dk. Bashiru alisema tatizo hilo la siasa za ugomvi, liliibuka katika vyama vyote wakati wa uchaguzi mkuu, lakini tatizo lilikuwa kubwa zaidi CCM.


Alisema pia wanachama wengi wa chama hicho waliondoka kwa sababu kilitengeneza mfumo ambao bila kuwa na fedha ni vigumu kupata uongozi na kwamba baadhi walitaka vyeo ili wapange safu zao.

Kuhusu kuhama kwa wabunge, madiwani na viongozi wengine wa upinzani na kujiunga na CCM, alisema vyama husika vijitathimini kwanini watu hao waondoke kwao.


“Iweje ndani ya muda mfupi vinakimbiwa na wanachama na kukimbilia mahala pengine?” alihoji.


Dk. Bashiru alipoulizwa kama anadhani ni muhimu nchi ikarudi kwenye mfumo wa chama kimoja, alisema; “wingi wa vyama siyo demokrasia, umadhubuti wa mfumo wa vyama vingi ndiyo suala muhimu.


“Bado mfumo wetu wa vyama vingi ni legelege na vyama havijakua kitaasisi, hata CCM bado inabidi kuimarishwa kuwa chama madhubuti.”


Alisema hata kama vyama vitapukutika na kubaki viwili, haoni kama ni faida au hasara kwa kuwa itategemea vinavyobaki vinatoa mchango gani na kwamba kinachohitajika ni wananchi kuamua.


Credit: Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527