KANGI LUGOLA ATOA SIKU 15


Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akisisitiza jambo.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola ametoa siku 15 kwa kampuni saba zilizobainika kufanya ufisadi katika mradi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kurejesha Sh28.5bilioni walizolipwa, ili kuepuka kuwa wateja wa mahakama ya mafisadi.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 4, mjini Dodoma ikiwa ni siku moja baada ya kukutana na wamiliki wa kampuni hizo kuomba wawasilishe vielelezo vya malipo hayo, ambapo amezitaja kampuni hizo kuwa ni Gotham International Ltd (Sh2.8 bilioni), Iris Corporation Berhard (Sh22.9 bilioni), Gwiholoto impex Ltd (Sh 946.4 milioni), Skyes Travel Agent (Sh6 milioni), Dk Shija Paulo Rimoy (Sh27 milioni), Aste Insurance (Sh1.2 bilioni) na BMTL (Sh 569.1 milioni) ambayo imekubali kurejesha fedha hizo.

“Takwimu nilizonazo mahakama ile ya mafisadi bado ina uhaba wa mafisadi, mimi nina dhamana ya kuitafutia wateja. Nyinyi tuliohojiana muombe msiwe miongoni mwa wateja ninaoitafutia mahakama hiyo, na msilete mchezo na serikali hii ya awamu ya tano”, amesema Lugola

Kuhusu hatima ya aliyekuwa mkurugenzi wa Nida, Dickson Maimu na kampuni ya Iris Corporation Berhard ya nchini Malasia ambayo ililipwa Shilingi bilioni 32 na Nida kwa ajili ya kuleta mtambo wa kutengenezea kadi ghafi nchini, amesema itajulikana Agosti 17, 2018.

“Maimu ametusaidia kupata maelezo ya ziada kuhusu ile kampuni,baada ya siku 14 watakavyokuja ndio tutajua hatima yake, tutajua kama suala litaisha ama la,” amesema Lugola.

Julai 25, 2018 Lugola aliipa wiki mbili kampuni ya Iris na Ghotham kwenda ofisini kwake kujadiliana jinsi ya kumaliza suala hilo, ambapo jana Maimu na mmiliki wa kampuni ya Jack Ghotham waliitika wito wake na kutoa maelezo ya ziada ambayo yatawasaidia katika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Ufisadi huo katika mradi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), uligundulika katika ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Februari, 2016.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527