WAWILI WAFARIKI WAKISAKA DHAHABU TARIME

Watu wawili wamefariki dunia kwa kufukiwa na kifusi cha udongo wakati wakichimba madini ya dhahabu katika machimbo madogo yaliyoko mtaa wa Buguti Kata ya Turwa wilayani Tarime.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 6, 2018 Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema tukio hilo limetokea jana Jumapili Agosti 5 na kuwataja waliofariki kuwa ni Bisaku Chacha (19) na Charles Mairo (18).


Amesema marehemu waliingia kwenye shimo lililokuwa limeachwa kwa siku nyingi wakitafuta mawe ya dhahabu matokeo yake waliangukiwa na mawe hayo.

Mzazi wa Charles, Mairo Wembe amesema hakuziamini taarifa za mwanae kufariki dunia, baada ya kurejea nyumbani ndio aliamini.

Mkazi wa mtaa wa Kibuye kata ya Ketare, Werema Marwa amesema vijana hao waliondoka wenyewe na kuingia shimo ni bila kuwa na mtu mwingine nje na hata walipofukiwa na kifusi hicho walikosa msaada.

Amesema walishitukia tukio hilo saa 12 jioni baada ya kufika eneo hilo na kutambua viatu vyao na kuvichukua kuvipeleka nyumbani lakini walipoenda kuchunguliwa waliona miguu huku mwili ukiwa umefukiwa.

“Tuliita watu waje kutusaidia kufukua na kufanikiwa kuwatoa ndani ya shimo hilo,” amesema Marwa.

Hivi karibuni watu wengine watatu walifukiwa kwenye mgodi huo, mmoja kufariki dunia.

Na Waitara meng'anyi, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527