MBUNGE WA KISHAPU SULEIMAN NCHAMBI MBARONI KWA TUHUMA YA RUSHWA

Kulia ni Mbunge wa Kishapu Suleiman Nchambi akiwa na rais John Pombe Magufuli - Picha kutoka maktaba

Mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi na viongozi watatu wa mgodi wa Stamigold ulioko Tulawaka wilayani Biharamulo mkoani Kagera, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Biharamulo, Hassan Mosi amesema mbunge huyo na wenzake walikamatwa na kuwekwa rumande katika gereza la wilaya hiyo Jumamosi Agosti 4, 2018.


Amesema leo Jumatatu Agosti 6, 2018 watafikishwa mahakama ya wilaya ya Biharamulo kwa kosa la kufanya miamala ya kupokea rushwa.


Mosi amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha15 cha sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya kupambana na kuzuia rushwa.


"Wakifikishwa mahakamani watasomewa mashtaka yanayowakabili. Wanaweza kukiri au kukanusha na sheria itachukua mkondo wake,” amesema.


Ndugu, jamaa na marafiki leo wamejitokeza kwa wingi katika mahakama hiyo, huku wengi wakionekana kuwa na shauku ya kujua hatima ya viongozi hao.
Na Shaaban Ndyamukama, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527