ASKARI WANNE WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA RUSHWA

Askari wanne wa Pori la Akiba la Mkungunero, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kiteto kwa tuhuma ya kushawishi na kuomba rushwa ya Sh milioni tano kutoka kwa wafugaji ambao mifugo yao ilikamatwa ndani ya pori hilo.


Akisoma hati ya mashtaka ya watuhumiwa hao, Mwendesha mashataka wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Isdory Kyando mbele ya Hakimu Mkazi, Hudi Majid, alidai tukio hilo lilitokea Mei 12 mwaka huu katika Kijiji cha Ilkiushbouir wilayani Kiteto.


Kyando aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Martenus Mahoka, Augustino Sadick, Ephrahim Polepole na Godfrey Matheas wote askari wa Pori la Akiba la Mkungunero.


Alidai fedha hizo waliziomba kutoka kwa wenye mifugo waliokuwa wamekamatwa ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero waweze kuiachia mifugo199 wakiwamo ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda.


Kyando alidai washtakiwa hao kwa pamoja wanatuhumiwa kutenda kosa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007 kifungu cha 15 (1),


Washtakiwa hao kwa pamoja walikana mashitaka na walipata dhamana hadi Septemba 17 mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527