ALIYETAKA KUMHONGA WAZIRI LUKUVI MILIONI 90 AFIKISHWA MAHAKAMANI

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imempandisha kizimbani Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group. Co.ltd na Kiluwa Free Processing Zone, Mohamed Kiluwa (50) kwa tuhuma za kutoa rushwa ya Shilingi Milioni 90 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.


Mshtakiwa huyo amepandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi na kusomewa shtaka moja la kujihusisha na vitendo vya rushwa.


Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Shaidi, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka TAKUKURU, Maghela Ndimbo amedai July 16,2018 kati ya saa 6 na 8 mchana mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi wa kampuni hizo mbili alitoa rushwa ya Dola za kimarekani 40,000 sawa na Sh. Milioni 90 kwa Waziri Lukuvi.


Wakili Ndimbo amedai mshtakiwa huyo alitoa fedha hizo kwa lengo la kutowasilisha hati ya umiliki wa kiwanja namba 57 ‘Block B’ Kikongo na ‘Block D’ Disunyura kilichopo eneo la viwanda Kibaha mkoani Pwani.


Baada ya kusoma shtaka hilo, Wakili Ndimbo ameiomba mahakama kuwapangia tarehe ya kutajwa kwa shauri hiyo na kuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na hawana pingamizi kuhusiana na mshtakiwa huyo kupewa dhamana.


Naye Wakili Upande wa Utetezi Imani Madega amedai kuwa kwa kuwa upande wa mashtaka hauna pingamizi na dhamana dhidi ya mshtakiwa wanaiomba mahakama itoe dhamana kwa kuzingatia masharti.


Hakimu Shaidi amesema ili mshtakiwa huyo apate dhamana anatakiwa kuwa na wadhamini 2 na mmoja atoe fedha taslimu mahakamani hapo kiasi cha Sh. Milioni 45 na kama hana awasilishe hati ya mali isiyo hamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha, Masharti ambayo upande wa utetezi uliyatekeleza na mshtakiwa akaachiwa kwa dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi August 15,2018.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527