UFARANSA YATINGA FAINALI KOMBE LA DUNIA


Wachezaji wa Ufaransa wakifurahia baada ya mechi kumalizika.

Baada ya usiku wa Julai 10,2018 kushinda mechi yao ya nusu fainali dhidi ya Ubelgiji kwa bao 1-0, Ufaransa sasa imetinga fainali ya kombe la dunia kwa mara ya tatu ndani ya miaka 20 na kuwa taifa lililofika fainali mara nyingi zaidi katika miaka hiyo.

Ufaransa imefanikiwa kutinga hatua ya fainali katika miaka ya 1998 ambapo walitwaa kombe wakiwafunga Brazil kwenye mechi ya fainali, 2006 ambapo walifungwa na Italia na 2018 baada ya leo kushinda bao 1-0 dhidi ya Ubelgiji kwenye nusu fainali.

Kwa upande wake kocha wa kikosi hicho Mfaransa, Didier Deschamps, ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa Ufaransa kufika katika fainali mbili tofauti za mashindano makubwa. Alifika fainali ya EURO 2016 na kupoteza dhidi ya Ureno na amefika fainali ya kombe la dunia 2018.

Kwa upande mwingine walinzi wa kikosi cha Ufaransa mwaka huu Pavard, Varane na Umtiti wote wamefunga katika fainali hizi na kuirudia rekodi ya walinzi Lizarazu, Blanc na Thuram ambao walifunga mabao katika fainali za mwaka 1998. 

Naye Antoine Griezmann sasa amehusika kwenye mabao 5 akifunga 3 na kusaidia 2 hivyo kuwa nyuma ya Harry Kane pekee kama mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi katika fainali hizi. Kane amehusika kwenye mabao 6 yote akifunga.

Ufaransa sasa itasubiri mshindi wa nusu fainali ya pili itakayopigwa kesho kati ya Croatia dhidi ya England, ambapo mshindi ataungana na Ufaransa katika mchezo wa fainali utakaofanyika Julai 15.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527