NYOTA WALIOPAISHWA NA KOMBE LA DUNIA


Kutoka kushoto ni Hirving Lozano wa Mexico, Aleksandr Golovin wa Urusi na Juan Quintero wa Colombia.

Katika fainali za kombe la dunia mara zote huwa vinapatikana vipaji vipya ambavyo hupata nafasi ya kusajiliwa na klabu kubwa. Moja ya mifano ni James Rodriquez ambaye alisajiliwa na Real Madrid kutoka Monaco baada ya kufanya vizuri kwenye fainali za mwaka 2014.

Kwa mujibu wa wachambuzi mbalimbali wa soka duniani, fainali za mwaka huu hazijatoa vipaji vipya vya kuonekana moja kwa moja lakini kuna vipaji ambavyo vinaonekana kunufaika kutokana na viwango walivyoonesha na inaweza isiwe tabu kwa mawakala wao kuwauza kwenye timu kubwa.

1. Hirving Lozano, huyu ni nyota wa PSV Eindhoven ambaye ameonesha kiwango bora akiwa na Mexico. Ana miaka 22 na wakala wake ni Mino Raiola, ambaye ameripotiwa kuwa kwenye mazungumzo na klabu za Arsenal, Barcelona na Manchester United kukamilisha uhamisho wa nyota huyo.

2. Aleksandr Golovin, raia wa Urusi ambao walikuwa wenyeji wa fainali na kutokana na kiwango chake aliisaidia timu yake kufika hatua ya robo fainali. Anachezea CSKA Moscow na klabu ya Chelsea imeripotiwa kuhitaji huduma yake.

3. Wilmar Barrios na Yerry Mina, hawa ni nyota wa Colombia, Wilmar akicheza kiungo na Mina beki wameonesha ubora mkubwa na pengine kwa Mina kujihakikishia nafasi kwenye kikosi cha Barcelona huku Wilmar (24) anayechezea Boca Junior ya Argentina akivivutia vilabu vya Tottenham na PSG.

Kutoka kushoto ni Yerry Mina wa Colombia, Jo Hyeon-Woo wa Korea Kusini na Alireza Jahanbakhsh wa Iran.

4. Juan Quintero, huyu ni nyota mwingine wa Colombia anayechezea River Plate ya Argentina, ana miaka 25 na ameonesha kiwango kikubwa na sasa anatajwa kuwaniwa na klabu ya Real Madrid pamoja na Tottenham.

5. Alireza Jahanbakhsh na Milad Mohammadi, hawa ni nyota wa Iran ambao walilisaidia taifa hilo kuwashangaza wengi kwa kutoa upinzani mkubwa kwa timu za Hispania na Ureno katika kundi B. Alireza (24) ambaye ni winga wa AZ Alkmaar sasa anawindwa na vilabu vya Leicester City na AC Milan. Mlinzi Milad (24) yeye anatajwa kuhitajika na klabu za Celtic na Rangers.

6. Jo Hyeon-Woo, huyu ni mlinda mlango wa Japan anayechezea timu ya Daegu FC, kutokana na kiwango chake alichoonesha kwenye mechi za kundi F sasa anatajwa kuwaniwa na Liverpool.

Hao ni baadhi tu ya nyota ambao wanatajwa sana kwenye dirisha la usajili kutokana na viwango vyao kwenye kombe la dunia 2018, ambalo limemalizika Julai 15 kwa Ufaransa kuwafunga Croatia mabao 4-2 na kuibuka mabingwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527