MWANAMKE MBARONI KWA WIZI WA MTOTO MWANZA

Mwanamke mmoja anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa wiki tatu.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Paulina Mashiku (27) ni mkazi wa ukijiji cha Mbugani wilayani Sengerema.


Alisema mtuhumiwa huyo aliyekuwa ameolewa na mwanamume anayeishi maeneo ya Bukoba visiwani anakojishughulisha na uvuvi kwa kipindi chote cha ndoa yao hawajawahi kupata mtoto jambo lililosababisha mwanamke huyo kumdanganya mumewe kuwa amepata ujauzito.


Juzi, majira ya saa sita mchana alifanya kitendo hicho lakini siku mbili kabla ya tukio, alipita katika kijiji cha Buliyaheke na kumwona mwanamke akinyonyesha mtoto mchanga ndipo alipochukua jukumu la kumpigia simu mumewe na kuwaaga majirani anakwenda hospitalini kujifungua.


Alisema kesho yake alifika katika nyumba alipo mtoto huyo majira ya 4:00 usiku na kumwona mama wa mtoto akiwa nje akipika wakati huo mtoto akiwa amelala chumbani. Alipita mlango wa uwani na kumwiba mtoto huyo na kurudi naye nyumba kwake huku akiwaeleza majirani kuwa amejifungua salama.


"Jambo hilo liliwapa wasiwasi majirani kwa kuwa walipata taarifa katika kijiji cha Buliyaheke kuna mwanamke ameibiwa mtoto, hivyo wakatoa taarifa kituo cha polisi.


“Baada ya kupokea taarifa, polisi walifanya ufatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio kisha mtuhumiwa aliwekwa nguvuni na alipohojiwa alikiri ni kweli alimwiba mtoto," alisema Msangi


Aliongeza kuwa hali ya mtoto ni nzuri na tayari amekabidhiwa kwa mama yake mzazi na polisi wako katika mahojiano na mtuhumiwa. Alisema pindi uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.


Kamanda Msangi alitoa wito kwa wakazi wa Mwanza kuwa waangalifu na watoto wao dhidi ya watu wenye nia ovu huku akiwataka waendelee kutoa ushirikiano na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu mapema ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527