MTOTO WA DARASA LA SITA ARUKA UKUTA KUREJEA ALIKOOZWA

MTOTO wa miaka 14 aliyeozwa akiwa mwanafunzi wa darasa la sita, aliruka ukuta wa kituo ambapo alihifadhiwa na serikali usiku wa manane mwishoni mwa wiki, imeelezwa.


Mtoto huyo (jina tunalihifadhi kwa sababu za kimaadili) alichukuliwa na serikali hapa Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita na kuhifadhiwa katika nyumba salama, ambayo huhifadhiwa watoto wa kike waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia.

Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi na Maandalizi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Safia Rijal, alisema Idara ya Ustawi wa Jamii ilimtaarifu kuwa mtoto huyo alitoroka usiku wa kuamkia juzi kutoka kituo ambacho alihifadhiwa.

“Tuliamua kumchukua mtoto huyo na kumpeleka katika nyumba salama baada ya kupata taarifa kuwa wazazi wake wamemuozesha wakati umri alionao ni mdogo... hastahiki kuolewa,” alisema Rijal.

Mkurugenzi huyo alisema amesikitishwa na kitendo cha mtoto huyo kutoroka mahali salama, hasa kwa kuwa angeweza kuchukua maamuzi yasiyofaa na baadaye serikali kupata lawama.

Alisema baada ya kupata taarifa hiyo alifuatilia na kugundua kuwa mtoto huyo alikimbilia nyumbani kwa wazazi wake na kwamba yupo salama.

“Afadhali amekimbilia kwao. Je, angelikwenda kwahala (mahali) kusikojulikana? Ingekuwa mtihani mkubwa," alisema mkurugenzi huyo.

"(sasa) Niwaombe wasimamizi wa hii nyumba salama kuwa na uangalifu mkubwa kwa watoto wanaofikishwa hapo, kwa kuwa wengi wao huwa wameathirika kisaikolojia kutokana na matendo waliyofanyiwa.”

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) upande wa Zanzibar, Dk. Mzuri Issa alisema wakati umefika kubadilisha sheria kwa kuwa adhabu iliyowekwa kwa mzazi anayemwozesha mtoto wa kike katika umri mdogo haiendani na wakati.
“Adhabu ya faini ya Sh. 1,500 kwa mzazi atakayemwozesha mtoto wake ni ndogo sana kwa sasa wakati mzazi anapokea mahari ya zaidi ya Sh. 500,000... kweli atashindwa kutoa (Sh.) 1,500,”alisema Dk. Mzuri.

Alisema kima kidogo hicho kinatokana na Sheria ya Elimu ya mwaka 1982.

Aidha, Dk. Mzuri alizipongeza Wizara ya Elimu, Ustawi wa Jamii na Jeshi la Polisi kwa kuwashikilia wazazi wa mtoto huyo kwa tuhuma za kumwozesha akiwa na umri mdogo.

JESHI LA POLISI
Ofisa Ustawi wa Jamii na Hifadhi ya Mtoto, Ali Wadi Ame, aliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa Jeshi la Polisi linawashikilia wazazi wote wa mtoto huyo.

Tukio hilo lilitokea Magogoni Wilaya ya Magharibi B, Unguja na viongozi wa serikali walifika katika eneo hilo na kukuta tayari mtoto huyo ameozeshwa.

Ame alisema ni kinyume na sheria kuoza mtoto aliye na umri wa chini ya miaka 18.
Alisema kuwa mtoto anahitaji malezi mazuri na kupatiwa elimu ambayo itaweza kumsaidia katika maisha yake ya baadaye.

“Kitendo cha mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 kuolewa ni kosa kwa mujibu wa sheria,” alisema ofisa huyo.

Baba mzazi wa mtoto huyo (jina tunalihifadhi), alisema waliamua kumuoza mtoto huyo kwa sababu hataki tena kusoma na kwamba alitoroshwa nyumbani na mwanaume kwa muda wa siku mbili.
“Huyu mtoto hataki tena kusoma, tumeamua kumuozesha ili asije kututia aibu na kutuzalia watoto akiwa bado hajaolewa,” alisema mzazi huyo.

Rijal alisema kitendo cha mtoto kuozeshwa hakikubaliki kwani ni udhalilishaji na kuwakosesha watoto haki zao za msingi ikiwamo kupata elimu.

Aliitaka jamii kutokubali watoto kuozwa wakiwa bado na umri mdogo kwani kuna hatari ya kupata athari za kiafya baadaye hasa wakati wa kujifungua.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Magharibi B, Hamza Ibrahim Mahmoud, alisema serikali inalaani ndoa za umri mdogo na kuwataka wananchi wasikubali kuyamaliza mambo hayo wenyewe, mtoto anapotoroshwa au kubakwa na badala yake wafike katika vyombo vya sheria.

Aliliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta bwana harusi ambaye kwa sasa hajulikani alipo, ili achukuliwe hatua za kisheria kutokana na kumtorosha na kumuoa mwanafunzi.

Alisema Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein ameondoa gharama katika elimu hivyo hakuna sababu ya kumkosesha mtoto haki hiyo.
Chanzo- NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527