JINSI BARUA YA KKKT INAVYODAIWA KUMNG'OA MWIGULU NCHEMBA

RAIS John Magufuli jana alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kumng’oa Mwigulu Nchemba na kumteua Kangi Lugola kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Aidha, nafasi ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepata mtu mpya baada ya Meja Jenerali Projest Rwegasira kustaafu.


Taarifa ya Ikulu iliyosomwa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, haikutaja sababu za Rais Magufuli kumuondoa waziri huyo kutoka wizara hiyo.

Lakini hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilijikuta ikihatarisha utulivu wa nchi baada ya kuibuka kwa barua ya onyo kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), ambapo Mwigulu alilazimika kumsimamisha ofisa wa ngazi ya juu kupisha uchunguzi.

Serikali na taasisi za kidini zinashirikiana kwa karibu katika kutafuta maendeleo nchini, na Rais Magufuli ameshiriki katika hafla nyingi za madhehebu na dini mbalimbali akiwa mgeni rasmi.

Kufuatia taarifa ya jana, Lugola anakuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa tatu tangu Rais Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015.

Kabla ya Mwigulu ambaye amehitimu Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni, wizara hiyo iliongozwa na Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga aliyefukuzwa kazi Mei 20, 2016.

Akitangaza mabadiliko hayo, Katibu Mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi alisema Rais Magufuli pia amewabadilisha ofisi mawaziri mawili, ambapo Prof. Makame Mbarawa atakuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Isaac Kamwele kuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

“Rais amefanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri kwa kufanya uteuzi wa waziri mmoja, manaibu mawaziri wawili na kuwabadilisha wizara mawaziri wawili,” alisema Balozi Kijazi.

Mapema mwezi uliopita, Mwigulu alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.

Aidha, siku hiyo Mwigulu alisema barua inayodaiwa kuandikwa na serikali dhidi ya "makanisa" iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandaoni ya kijamii si ya kweli na kwamba ni uhalifu uliofanywa na watu wasioitakia nchi mema.

Waziri huyo wa zamani alisema zaidi kuwa Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo, mazungumzo hufanyika na si kuandikiana barua kama ilivyofanywa katika taarifa hiyo iliyosambaa.

“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo taarifa hiyo inayosambaa ni batili na tayari uchunguzi umeanza kufanyika," alisema Mwigulu Juni 8.

"Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo.”

NAIBU WAZIRI
Pia, katika mabadiliko hayo ya jana, Rais Magufuli alimteua Mussa Sima (Mbunge wa Singida Mjini) kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, na kumteua Omary Mgumba (Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki) kuwa Naibu Waziri Wizara ya Kilimo ili kuongeza nguvu wizara hiyo, Balozi Kijazi alisema.
Kadhalika, Balozi Kijazi alisema Rais Magufuli amefanya uteuzi wa makatibu wakuu watatu pamoja na manaibu makatibu wakuu wanne.

Aliwataja makatibu wakuu walioteuliwa kuwa ni Moses Kusiluka kuwa Katibu Mkuu Ikulu akichukua nafasi ya Alphayo Kidata aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.

Mwingine ni Dk. Rashid Tamatama aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Uvuvi na Meja Janerali Jacob Kingu kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Rwegasira.
Balozi Kijazi aliwataja Manaibu Makatibu Wakuu walioteuliwa kuwa ni Balozi Joseph Sokoine kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais na Ramadhan Kailima kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani.

Wengine ni Prof. Siza Donald kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mathias Kambulugulu kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kadhalika, Balozi Kijazi alisema Rais Magufuli amefanya uteuzi wa balozi kwa kumteua Hassan Yahaya ambaye atapangiwa kituo cha kazi baadaye.

Aidha, Rais amemteua Athuman Kiamia kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), alisema. "Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha".

Alisema, pia Rais Magufuli amewateua makamishna wa Nec, kwa kumteua Jaji Mbaruku Salim kuwa kamishna wa Nec na kuwa Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo na Balozi Ramadhan Mapuri.

CHANZO- NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527