MFANYABIASHARA ZACHARIA ANYIMWA TENA DHAMANA KESI YA KUJARIBU KUUA

Matumaini ya Mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa, Peter Zakaria kupata dhamana na kuungana na familia yake yameyeyuka baada ya kurejeshwa rumande kwa kukosa dhamana katika moja ya mashtaka mapya mawili aliyosomewa leo.


Wakati akisubiri uamuzi wa Mahakama kuhusu dhamana yake katika kesi ya kujaribu kuua kwa kuwapiga risasi Ahmed Segule na Isaac Bwire, leo Julai 10,2018 Zakaria amejikuta akisomewa shtaka jipya la kumiliki bunduki aina ya shortgun na risasi tano kinyume cha sheria.


Licha ya kuachiwa kwa dhamana katika shtaka la kujaribu kuua, mfanyabiashara huyo amejikuta akirejeshwa mahabusu baada ya Wakili wa Serikali, Samuel Lukelo kupinga dhamana yake katika kesi ya kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria.


Juhudi za mawakili wa Zakaria, Kassim Gila na Onyango Otieno kuishawishi Mahakama mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi, Rahim Mushi kumpa dhamana mteja wao leo hazikuzaa matunda baada ya shauri hilo kuahirishwa hadi Julai 12 uamuzi kuhusu dhamana hiyo utakapotolewa.


Katika shtaka la kwanza, Zakaria anayemiliki kampuni ya mabasi ya Zakaria yanayosafiri kati ya mikoa ya Mwanza, Simiyu na Mara anadaiwa kujaribu kuwaua kwa kuwapiga risasi Segule na Bwire wanaodaiwa kuwa ni maofisa usalama wa taifa katika tukio lililotokea Juni 25 eneo la kituo cha mafuta kinachomilikiwa na Zakaria mjini Tarime.


Mahakama imemuachia kwa dhamana katika shauri hilo baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini watatu, wawili wakiwa watumishi wa Serikali waliosaini hati ya dhamana ya Sh10 milioni.


Awali mshtakiwa alifikishwa mahakamani Julai 5 na kusomewa mashtaka hayo ambapo leo mahakama ilipanga kutoa uamuzi kuhusu dhamana.


Katika shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa kumiliki bunduki aina ya shortgun na risasi tano kinyume cha sheria. Kosa hili halikuwa na dhamana na amerudishwa rumande hadi Julai 12.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527