Tuesday, July 3, 2018

HISTORIA NA UMAARUFU WA STEPHEN NGONYANI 'PROFESA MAJI MAREFU'..KUZIKWA JULAI 5

  Malunde       Tuesday, July 3, 2018
Moja ya matangazo ya Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu enzi za uhai wake - Picha kutoka Maktaba
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu atakumbukwa kwa mengi. Pichani akiwaokoa mtu na mtoto wake mara baada ya kuzingirwa na maji ya mafuriko yaliyotokea kwenye Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo wilayani Korogwe Mei 11, 2017. Kila mtu alishangazwa na ujasiri huo, wakati kwa kitendo hicho alichofanya kilikuwa kinahatarisha maisha yake. (Picha na Maktaba).
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu enzi za uhai wake

Mbunge wa Korogwe Vijijini kupitia CCM Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Maji Marefu ameaga Dunia jana Julai 2,2018.

Taarifa zinasema Maji marefu alikuwa amelazwa Dodoma kwa matibabu na June 20 akahamishiwa katika hospitali ya taifa ya muhimbili kabla mauti kumkuta.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na uongozi wa hospitali ya Muhimbili.

Ikumbumkwe kuwa mapema tarehe sita mwezi June mwaka huu Profesa Maji marefu alifiwa na mke wake aliyekuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya taifa Muhimbili.

Stephen Hilary Ngonyani amezaliwa mwezi mei mwaka 1956, amekuwa mbunge wa Korogwe vijijini tangu mwaka 2010.

Alizidi kupata umaarufu katika ulimwengu wa siasa.

Katika harakati zake za kutetea wananchi Bungeni, mwaka 2016 Ngonyani alitoa hoja ya kupandisha bei ya petrol na kushusha bei ya sukari ili kuwasaidia zaidi watanzania hasa wa hali ya chini.

Kabla ya hapo Ngonyani alifahamika zaidi kama profesa Maji marefu ambapo alikuwa ni mganga na mtaalamu wa tiba za asili.

Shughuli zake za uganga zili zungumziwa katika mitandao na hata baadhi ya majarida.

Nchini Kenya Stephen Ngonyani ama profesa Maji marefu, aliwahi kuweka kituo cha kazi zake za tiba Kenya na alifanya kazi kama mganga wa kienyeji.

Alimulikwa mnamo mwaka 2010 baada ya kuhusishwa katika mgogoro wa familia ya aliyekuwa mwana siasa maarufu na tajiri.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Hillary Ngonyani ambaye ni Msemaji wa Familia (kaka wa marehemu) alisema Majimarefu alizaliwa mwaka 1956 kwenye kijiji cha Kwamndolwa katika Halmashauri ya Mji Korogwe na kupata elimu yake ya msingi Kwamndolwa hadi alipomaliza mwaka 1975 na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari.

Ngonyani alisema tangu wakati huo, Majimarefu amekuwa mjasiriamali wa shughuli mbalimbali na hasa upande wa michezo, huku akipiga madisko kwenye kumbi mbalimbali hadi alipoanza tiba za asili mwaka 1990 hadi kifo chake, huku akibatizwa jina la Majimarefu kutokana na uwezo wake wa kupambana na wachawi.

Kabla ya kugombea ubunge mwaka 2005 kisha kupigwa chini na baadae kuja kushinda mwaka 2010, tayari huko nyuma aliwasaidia baadhi ya watu kupata ubunge na nafasi mbalimbali kwenye maisha kutokana na umaarufu wake.

Ukiacha ubunge ambao amekuwa nao hadi kifo chake, pia amewahi kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa, Katibu wa Uchumi na Fedha wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na hadi kifo chake ni Mbunge na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi kupitia wabunge wa CCM hadi 2021.


"Huyu bwana (Majimarefu) alikuwa na kipaji, na nataka kusema, uongozi ni kipaji sio elimu peke yake. Elimu bila kipaji ni kazi bure. Hata hivyo amerithi kutoka kwa babu yake mzaa mama mzee Enzi Mapunda, kwani alikuwa Zumbe (Mtawala wa eneo fulani, iwe ukubwa wa kata, tarafa ama wilaya) huko Kwamndolwa wakati wa Ukoloni" alisema Ngonyani.


Ngonyani alisema Majimarefu amefariki Juni 2, 2018 saa tatu usiku kwenye chumba namba moja cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Muhimbili, na alikuwa anasumbuliwa na Homa ya Mapafu kwa muda mrefu.

"Pamoja na kuumwa arnimonia kali (homa ya mapafu), mara chache alikuwa anasumbuliwa na presha ya kushuka. Kabla ya hapo alikuwa anasumbuliwa na nyonga, na hiyo ilimfanya alazwe nchini India mwezi mmoja" alisema Ngonyani ambaye yeye ndiyo aliyemlea Majimarefu.


Ngonyani alisema  Julai 4,2018 mwili utaagwa kwenye viwanja vya Bunge la kwanza la Tanganyika, Karimjee kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kabla ya kuanza safari ya kwenda Korogwe kwa mazishi. Alisema msiba utakuwa nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Masuguru mjini Korogwe maarufu kama Mamba Club.

"Mazishi yatakuwa Julai 5, 2018 siku ya alhamisi saa 10 jioni kwenye makaburi ya kijiji cha Kwamndolwa. Ni baada ya kuswaliwa saa saba mchana kwenye Msikiti Mkuu wa Ijumaa mjini Korogwe" alisema Ngonyani.


Ngonyani alisema, Majimarefu ameacha wake wawili Salma na Halia. Ni baada ya hivi karibuni kufiwa na mke mkubwa Bi. Mariam, huku watoto wakiwa 11, watoto wa kike sita na kiume watano.


Na kati ya watoto hao wa kiume, mmoja ana siku tano tangu kuzaliwa kwake, na amepewa jina la Hillary ambaye ni baba yake mkubwa.
Imeandaliwa na Yusuph Mussa - Malunde1 blog
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post