LESENI 878 FEKI ZA MADEREVA ZAKAMATWA

Jumla ya leseni 878 kati ya 73,904 za magari mbalimbali madereva wake wamebainika kuzitumia daraja lisilostahiki.


Leseni hizo ni zile zilizokaguliwa kuanzia Julai 4 hadi 15, mwaka huu katika ukaguzi maalumu uliofanywa wa kukagua leseni hizo.


Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu amesema hayo jijini Dar es Salaam leo Jumanne Julai 24.


“Kwa madereva wote watakaobainika kuendesha magari bila leseni stahiki kulingana na magari wanayoendesha, watakamatwa na kufikishwa mahakamani na leseni zao zitafungiwa kwa kigezo cha kukosa sifa ya kuendesha magari hayo,” amesema.


Aidha, Kamanda Musilimu ametoa muda wa wiki moja kwa madereva wanaodaiwa na mfumo wa Usimamizi wa Trafiki kulipa madeni yao yote.


Amesema baada ya muda huo uliotolewa kupita wataanza msako nchi nzima kukamata madereva wanaodaiwa na kuwapeleka mahakamani na gari zao zitazuiliwa. 

Kamanda Musilimu pia amesisitiza kuwachukulia hatua abiria wanaowashawishi madereva kuongeza mwendo wa gari wawapo safarini.


“Abiria watakaochochea ajali za barabarani kwa kuwaambia madereva waongeze mwendo watachukuliwa hatua, inapaswa abiria kutoa taarifa waonapo uvunjwaji wa sheria,” amesema. 


Pamoja na mambo mengine, amesema Agosti Mosi mwaka huu, askari wa usalama barabarani watafanya uhakiki wa kina wa leseni za madereva kwa madereva wa magari ya abiria, mizigo, magari binafsi, pikipiki na magari ya serikali nchi nzima.


“Tutakuwa na fomu husika kwa ajili ya uhakiki wa leseni za madereva fomu hizi zitakaa katika vituo vya daladala (stendi) na katika vituo vya mizani hii itapunguza kurudia rudia ukaguzi wa leseni kwa madereva,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527