JINSI ASKOFU ALIVYOTIKISA VIONGOZI, TAASISI KWA UTAPELI | MALUNDE 1 BLOG

Monday, July 23, 2018

JINSI ASKOFU ALIVYOTIKISA VIONGOZI, TAASISI KWA UTAPELI

  Malunde       Monday, July 23, 2018

Askofu Mkuu wa Kanisa la Agape Martin Gwila(wa pili kushoto)akiteta jambo na baadhi ya viongozi mara baada ya kuwasili katika kijiji cha Musati.Picha na Maktaba.


 Hawakuwa na sababu ya kutomwamini; si tu kwa sababu ni kiongozi wa dini, bali kutokana na uwezo mkubwa wa ushawishi alionao.

Alipowashawishi walipe kwenye akaunti yake Dola 2,500 za Marekani (takriban Sh5.6 milioni) ili awapeleke Israel kuonana na mfadhili wa kanisa lake, hakuna aliyeshtuka kuwa wangeishia kutapeliwa.


Hakusita hata ‘kuwaingia’ viongozi wa juu wa Serikali, maskofu wenzake, wakandarasi na viongozi wastaafu ambao sasa wanaugulia majeraha ya kutapeliwa.


Huyu ni Askofu Martin Gwila, mkuu wa Kanisa la Agape Sanctuary International, tawi la Tanzania anayechunguzwa kwa utapeli.


Tayari Askofu Gwila amekwishashtakiwa kwa udanganyifu katika kesi mbili tofauti akidaiwa kuwatapeli watu mbalimbali na taasisi mamilioni ya fedha na mali.


Kwa zaidi ya wiki mbili Mwananchi halikufanikiwa kumpata kiongozi huyo wa dini, lakini baadhi ya watu wanaodai kutapeliwa wamejitokeza na kueleza jinsi ‘alivyowaingiza majini’.


Taarifa ambazo gazeti hili limezikusanya zinaeleza kuwa Gwila amewahi kumtapeli kiongozi wa juu wa moja ya mihimili mitatu ya dola nchini.


“Shutuma zote za utapeli za mchungaji huyo ni za kweli, ila ningeshauri mambo yangu yasiwekwe hadharani kwa sasa, inatosha tu kukuambia shutuma dhidi yake ni za kweli,” alisema kiongozi huyo mkubwa nchini.


Ujanja anaoutumia askofu huyo ni kuwalaghai watu kuwa kuna mfadhili kutoka Brazil ambaye amekubali kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kanisa hilo nchini.


Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa makanisa, vyuo vikuu, hospitali na vituo vya kulea watoto yatima.


Mmoja wa watu ‘waliongizwa mjini’ na Gwila ni mmiliki wa Kampuni ya ujenzi ya Works Contractors, Michael Nyange, anayedai kutumia zaidi ya Sh100 milioni kutekeleza mradi wa ujenzi wa kanisa ya askofu huyo jijini Arusha bila malipo.


“Alitangaza tenda ya kujenga makanisa yake na tukapewa kazi na baada ya kutushawishi tukamwamini na kukubaliana malipo yatafanyika mwisho wa mradi. Hivi tunavyoongea sijalipwa. It is a bid setback to our business (ni pigo kubwa sana kwa biashara yetu),” anasema Nyange.


Kana kwamba hiyo haitosha, askofu huyo alifanikiwa kuwashawishi baadhi ya wakandarasi waliokuwa wakimdai kuwa walitakiwa kuweka kwenye akaunti yake $2,500 ikiwa ni gharama za kuwapeleka Israel kuonana na mfadhili wake ili wazungumze namna atakavyowalipa.


“Alitushawishi kuwa mfadhili anaye-finance (anayegharamia) miradi alipenda kukutana na contractors (wakandarasi), tukapewa akaunti ambayo tuliweka $2,500 lakini safari ile ikayeyuka na pesa hatukuzipata,” alisema Nyange.


Simu ya Askofu Gwila haikupatikana alipopigiwa na juhudi za kumpata katika maeneo anayoelezwa kuwa huwa anapatikana hazikuzaa matunda.


Kwa mara ya mwisho askofu huyo alionekana kwenye mkutano wa waandishi wa habari wa kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto. Katika mkutano huo Muroto alielezea tuhuma kadhaa zinazomkabili Gwila.
Makandarasi walizwa mabilioni


Nyaraka ambazo Mwananchi limezipata zinaonyesha kuwa kuna kundi la wakandarasi wanaomdai askofu huyo zaidi ya Sh28 bilioni walizopaswa kulipwa baada ya kupewa kazi ya kujenga makanisa 100 Tanzania Bara na Zanzibar.


Baadhi ya wakandarasi hao wameliambia gazeti hili kuwa ahadi kemkem na za kutamanisha walizopewa na askofu huyo ziliwashawishi kuanza kazi ya ujenzi bila kulipwa chochote.


Kana kwamba hiyo haitoshi, Askofu Gwila alifanikiwa kuwashawishi wakandarasi hao kuchanga fedha nyingine kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kazi zao kwa ahadi kuwa fedha hizo zitalipwa pamoja na zile za ujenzi wa makanisa.


Hadi habari hii inaandikwa hakuna mkandarasi hata mmoja aliyekwishalipwa licha ya wengi wao kukamilisha kazi miezi kadhaa iliyopita.


Chini ya mkataba walioingia na kanisa hilo, kila mkandarasi alipaswa kulipwa Sh284 milioni kwa kila kanisa analopaswa kujenga.


Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wakandarasi hao alisema baadhi yao wamefilisika kutokana na kufanyishwa kazi bila kulipwa.


“Tulilazimika kutumia fedha zetu, wengine walikopa, wengine wakatumia akiba zao kwa sababu tuliamini kuwa mtu wa kanisa hawezi kutufanyia hivi. Lakini sasa miezi mingi imepita baada ya kukamilisha kazi, tumeshaandika barua nyingi kudai fedha zetu bila mafanikio,” alisema mkandarasi mwingine aliyeomba kutoandikwa jina gazetini.


Gazeti hili limepata nakala kadhaa za nyaraka za madai ya wakandarasi hao zilizowasilishwa kwa Askofu Gwila kwa ajili ya malipo.


Pia, lina nakala za mlolongo wa barua kutoka kwa askofu huyo akiahidi kuwalipa wakandarasi hao mara fedha zitakapopatikana kutoka kwa mfadhili wake.


Katika kila barua, askofu huyo amekuwa akiwapa wakandarasi hao matumaini ya kulipwa “hivi karibuni” kwa kuwa fedha kwa ajili ya malipo tayari zimeshapatikana.


Wakandarasi wanaodai kudhulumiwa wamefungua malalamiko polisi wakitaka askofu huyo akamatwe na kushtakiwa kwa kuwatapeli.


Ofisa mmoja wa polisi amethibitisha kuwa tuhumu dhidi ya askofu huyo zimeripotiwa na zimeanza kuchunguzwa na Kitengo cha Uhalifu wa Kifedha (Financial Crime Unit) chini ya mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI). “Amewaibia watu wengi ndani ya nchi. Ni tapeli mkubwa na bado tunakusanya ushahidi na tumeanza kufanya taratibu ili kumleta Dar ajibu tuhuma,” alisema ofisa huyo.


Licha ya kutolipwa fedha za ujenzi wa makanisa, wakandarasi walioajiriwa na Askofu Gwila walilaghaiwa wakamlipa askofu huyo mamilioni ya fedha kwa ahadi nyingine nono.


Alifanikiwa kumshawishi kila mkandarasi kulipa Sh3 milioni zitumike kufanya maandalizi ya awali ya mradi kwa sababu kanisa lilikuwa halijapokea fedha kwa ajili ya kuanza kwa mradi huo.


“Kumbuka kuwa mradi ulihusisha takriban makanisa 100, hivyo hapa jumla alikusanya Sh300 milioni,” alisema mmoja wa wakandarasi hao.


Baadaye, wakandarasi hao walitakiwa kutoa Sh600,000 kila mmoja kama ada ya kuwezesha ziara yao ya mafunzo nchini Israeli na Brazil ambako mfadhili wa askofu huyo anayetajwa kwa jina la Joel Angel anaishi.


Katika mradi huo, Askofu Gwila na kanisa lake walimtumia mtumishi mmoja wa umma (jina tunalo) kama meneja na mshauri mkuu wa mradi.


Mtumishi huyo ambaye ni mhandisi wa halmashauri moja hapa nchini, ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa mradi na kuna baadhi ya barua kwenda kwa wakandarasi hao zimesainiwa na yeye.
Viongozi wa Serikali walivyozwa


Katika mlolongo wa matukio ya ulaghai wa askofu huyo ambaye anachunguzwa na polisi kwa tuhuma kadhaa za utapeli, alijaribu kumuingiza mjini mmoja wa viongozi wa juu kabisa nchini.


Kiongozi huyo alikubali kutoa ardhi yenye ukubwa wa eka 650 katika kata moja mkoani Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu cha mafunzo ya madaktari na wataalamu wa afya. Ujenzi huo haujawahi kuwepo.
Polisi Dodoma wamnasa


Mara ya mwisho, askofu huyo alipoonekana mbele ya wanahabari akiwa chini ya ulinzi wa polisi, kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Muroto alimuelezea kuwa anakabiliwa na tuhuma kadhaa za utapeli.


Muroto alimleta askofu huyo mbele ya waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa anatuhumiwa kuwatapeli watu mbalimbali na kujipatia zaidi ya Sh68 milioni kwa kuwapa ahadi ya kuwaajiri, lakini akashindwa kufanya hivyo.


Juzi, Muroto ameliambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa bado wanaendelea kumchunguza mchungaji huyo huku akikataa kueleza kwa kina uchunguzi huo unalenga nini.
Mwigulu naye alilaghaiwa?


Aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba yumo kwenye orodha ya viongozi walioongopewa na Askofu Gwila.


Huku akiamini kuwa Kanisa la Agape Sanctuary International lilikuwa limesajiliwa kutoa huduma hapa nchini, Dk Mwigulu alikubali kuwa mgeni rasmi katika moja ya mikutano iliyoandaliwa na askofu huyo.


Katika ghafla hiyo, waziri huyo alishawishiwa na miradi aliyoiorodhesha askofu huyo kutekelezwa na kanisa lake na Mwigulu kuchangia Sh1 milioni na mifuko 50 ya saruji.


Hata hivyo juhudi kadhaa za kumpata Dk Mwigulu kuelezea suala hilo hazikuweza kuzaa matunda, ingawa picha mbalimbali zilizowekwa kwenye mtandao zinamuonyesha mbunge huyo wa Iramba Magharibi akiwa ndani ya kanisa hilo alipoalikwa na Askofu Gwila kufungua semina ya viongozi wa kanisa lake.
Waziri wa zamani amkimbia


Wakati fulani, waziri wa zamani wa Ujenzi katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Nalaila Kiula alikuwa mshauri wa Askofu Gwila katika masuala ya kijamii na taratibu za Serikali, lakini anadaiwa kukaa naye mbali baada ya kugundua mwenendo wake usioridhisha.


“Ni kama miezi mitatu imepita tangu niamue kuachana na kuwa mshauri (wake), sijamwambia rasmi (Askofu Gwila) kwa sababu alikuwa polisi, nilikuwa nasubiri atoke ndiyo nimweleze,” alisema Kiula katika mahojiano na gazeti hili.


“Ulikuwa kama mkataba wa kienyeji kwa sababu hatukusainishana popote, yalikuwa ni makubaliano ya mdomo tu. Kwa kiasi kikubwa ushauri wangu ulikuwa ni katika mambo ya kijamii kutokana na uzoefu wangu wa kufanya kazi serikalini.”


Alipotakiwa kuelezea tuhuma zinazomkabili askofu huyo za kuwatapeli watu mbalimbali na taasisi, Kiula alisema hawezi kulisemea hilo kwa sasa kwa sababu liko chini ya uchunguzi wa polisi.
Kilio cha wachungaji


Utapeli wa askofu huyo haujawaacha salama watu walio karibu naye wakiwemo wachungaji wake.


Wachungaji hao wamefikia hatua ya kuandika waraka kuhusu mgogoro kati ya uongozi wa mikoa wa kanisa hilo dhidi ya askofu wao mkuu kwenda kwa Serikali.


Katika waraka huo ambao Mwananchi lina nakala yake, wachungaji hao wameorodhesha madai kadhaa yakiwamo kutapeliwa zaidi ya Sh1 bilioni na Askofu Gwila na baadhi yao kufukuzwa kazi katika mazingira yenye utata.


Lakini lililo kubwa katika waraka huo ni madai kuwa kanisa hilo halijasajiliwa kihalali hapa Tanzania kama kanisa, bali kampuni ya mtu binafsi.


Wanazitaja baadhi ya ahadi ambazo walipewa na askofu huyo kuwa ni pamoja na kuwajengea wachungaji wote nyumba zao binafsi, kuwajengea makanisa pamoja na ununuzi wa viwanja vya makanisa hayo, kutoa posho kwa wachungaji na watendaji wa kanisa, kutoa ufadhili kwa watoto wa kanisa na kujenga taasisi za huduma kwa jamii kama hospitali, shule na kumbi mbalimbali.


Wanabainisha kuwa waligundua utata katika usajili wa kanisa hilo baada ya wenzao sita kufukuzwa Mei 2016.


Wanasema baada ya kupata andiko la usajili wa Agape (Wuema) Sanctuary Ministries International Limited, ndipo walipobaini kuwa taasisi hiyo haijasajiliwa kama kanisa bali kampuni ya mtu binafsi.


“Yaliyo ndani ya mkataba huo sisi viongozi wa kanisa yemetusikitisha sana kwani hayaakisi kile tulichoaminishwa na kuthibitishiwa awali,” wanasema wachungaji hao.


Aidha, wachungaji hao wameorodhesha kwa ufupi baadhi ya fedha walizotoa wao, maaskofu, waumini na watu binafsi baada ya kutakiwa kufanya hivyo na askofu huyo.


Kila mchungaji aliyejisajili alilazimika kulipa Sh30,000, wengine Sh50,000, wengine Sh150,000 huku vijana zaidi ya 3,000 walioahidiwa ajira wakitakiwa kutoa Sh10,000 kila mmoja.
Wasaka ajira


Zaidi ya watu 800 ambao walitakiwa kuajiriwa kama walinzi walitoa Sh65,000 kila mmoja na kila mkandarasi aliyejaza mkataba wa ujenzi alipaswa kutoa Sh3.1 milioni.


Pia kuna watoto zaidi ya 4,000 wanaoishi katika mazingira magumu ambao walilipishwa Sh3,000 kila mmoja kwa ahadi ya kupatiwa ufadhili, lakini hakuna aliyepata ufadhili hadi leo.


Inaelezwa pia kuwa wachungaji, maaskofu na baadhi ya wakandarasi walitoa michango inayofikia Sh60 milioni kwa Askofu Gwila kwa ahadi ya kuwapeleka Israeli kwenye ziara ya mafunzo. Hadi sasa hakuna aliyepelekwa Israel.


“Inakisiwa kuwa mpaka sasa fedha zote alizopokea ni zaidi ya Sh1 bilioni kwa uchache sana,” inasema sehemu ya waraka huo ambao umeorodhesha majina 29 ya wachungaji waliouandaa.


Wachungaji hao wameiomba Serikali kusaidia kulichunguza kanisa hilo na hasa Askofu Gwila kwani juhudi zao za kuhoji zimegonga mwamba.


Mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo, Godson Nyirenda wa Dodoma, amethibitisha kushiriki kuandaa waraka huo na wenzake watatu kwa niaba ya wenzao 29 na kuwasilisha malalamiko hayo kwa msajili wa kiraia na waziri wa Mambo ya Ndani.


Ingawa Nyirenda hakupenda kueleza kinagaubaga walipewa majibu gani kutoka kwa msajili, hivi sasa wameanza mchakato wa usajili rasmi wa kanisa hilo.


Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa watu waliowahi kufanya kazi katika makao makuu ya kanisa hilo mkoani Arusha, alisema katika kipindi alichokaa hapo alishuhudia “mambo mengi ya ajabu ambayo siwezi kuyaelezea” kiasi cha kuamua kuondoka.


“Niliacha kazi katika kanisa hilo mwezi Agosti mwaka jana baada ya kuona vitu haviendi kama inavyopaswa, mambo mengi yalikuwa yanaendeshwa hovyo,” alisema mhasibu huyo wa kanisa wa zamani aliyejitambulisha kwa jina moja la Suzan.


Kwa mujibu wa Suzan, ofisi za kanisa hilo zilikuwa zikiendeshwa chini ya mamlaka ya mtu mmoja ambaye alikuwa hajali kufuata mambo ya msingi ya uendeshaji wa ofisi.


Suzan alisema, kwa mfano, hakukuwa na nyaraka zozote kutoka kwa waliodaiwa kuwa ni wafadhili kuonyesha kuwa kweli wamekubali kutoa fedha zitakazotumika kuendesha miradi mbalimbali.
Soma zaidi <<HAPA>>
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post