CHADEMA WAMSHUKIA KAMANDA MAMBOSASA KIFO CHA MWANAFUNZI ‘AKWILINA’

Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limesema kauli ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ya kukihusisha Chadema na mauaji ya mwanafunzi Akwilina Akwiline, inalenga kukiwekea chama hicho vikwazo kwenye uchaguzi mdogo wa Agosti 12.


Akizungumza na wanahabari jana, Kamanda Mambosasa alisema askari waliokuwa wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na kifo cha mwanafunzi wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) waliachiwa huru baada ya ushahidi kuwa hafifu.


Mambosasa alinukuliwa akisema, badala yake waliohusika ni Chadema waliohamasishaji maandamano yale ya kisiasa yaliyofanyika Februari 16, siku moja kabla ya uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni.


Akwilina alipigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala wakati viongozi na wanachama wa Chadema wakiandamana kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni.


Akizungumza na wanahabari leo Julai 25, Mwenyekiti wa Bavicha Patrick Ole Sosopi amesema kauli ya Mambosasa inalenga kuwaaminisha wananchi kuwa shughuli za Chadema ni hatari na sio salama kwa watu kuhudhuria.


"DPP (Mkurugenzi wa mashtaka) alishafunga jalada la kesi ya Akwilina, lakini Mambosasa ameliibua upya tena wakati ambao tunaelekea katika uchaguzi ili kuonyesha kuwa maandamano yanasababisha mauaji. Propaganda kama hizi alitakiwa kuzifanya Polepole (Katibu Mwenezi wa CCM) na sio mtendaji wa chombo cha dola," amesema Ole Sosopi.


Amesema hata leo yakiitishwa maandamano ya nchi nzima kama polisi hawatumii nguvu kuyazuia, hayawezi kusababisha mauaji kwa kuwa mtu hafi kwa kuandamana bali kwa kusababishiwa kifo hivyo polisi wafanye uchunguzi wa kutosha.


"Anasema viongozi wa Chadema waliokuwepo pale walikuwa na silaha, kama wao ndiyo walihusika waseme ni silaha ya nani iliyotumika kwani kuna maganda yaliyookotwa? Hivyo uchunguzi ukifanyika mhusika atabainika lakini katika mkutano ule polisi ndiyo waliokuwa na silaha za kivita," amesema Ole Sosopi.


Pia wametoa wito kwa wanafunzi wote nchi nzima na wazazi kulilia damu ya Akwilina mpaka pale haki itakapotendeka, lakini pia wao wataandika barua kwa balozi zote hapa nchini kuzitaarifu kuhusu hali ya ukandamizaji wa haki za binadamu ili wachukue tahadhari wawapo hapa.
Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527