ATUPWA JELA MIAKA MIWILI KWA WIZI WA MAKRETI MAWILI YA BIA


MAHAKAMA ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, imemhukumu Afred Emmanuel (41) kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na hatia ya wizi wa makreti mawili ya bia aina ya Balimi na Eagle. 

Mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Lalago wilayani Maswa.

Mbali na wizi huo alidaiwa kuiba fedha taslimu Sh. 137,000 mali za Mathayo Kisusi mkazi wa kijiji hicho.

Akitoa hukumu hiyo juzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Tumaini Marwa, alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka, hivyo kumpa adhabu hiyo. 

Mwendesha mashtaka wa polisi, Rashidi Achimtole, alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Julai, 8, mwaka jana, majira ya saa sita usiku.

Achimtole alidai kuwa siku na muda huo, mtuhumiwa alivunja dirisha la nyumba ya biashara mali ya Kisusi na kuiba kreti moja la Balimi lenye thamani ya Sh. 49,000, pamoja na kreti lingine la Eagle lenye thamani ya Sh. 22,000.

Mwendesha mashtaka huyo pia alidai kuwa mtuhumiwa pia aliiba fedha taslimu 137,000 hivyo kufanya vitu vyote alivyoiba kuwa na jumla ya thamani ya Sh. 208,000.

Alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume cha Sheria ya Makosa ya Jinai kifungu Na. 296(a) kinachosomwa sambamba na kifungu Na. 298 (1) na 265 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.

Kutokana na mahakama kumaliza kusikiliza mashahidi wa kesi hiyo wa upande wa mashtaka, mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo ili kuwa fundisho kwa watu wengine wenye nia ovu kama hiyo.

Kabla ya hukumu, Emmanuel alipewa nafasi ya kujitetea na kuomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa yeye anategemewa na familia lakini ombi hilo lilipingwa na mwendesha mashtaka.
Soma zaidi hap<<HAPA>>

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527