BEI YA DIZELI,PETROLI JUU


Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya ya mafuta kwa mwezi Julai ambapo bei ya petroli imeongezeka Sh126 kwa lita huku dizeli ikiongezeka kwa Sh166.


Kiwango hiki ni kikubwa zaidi kuwahi kutokea kwa mara moja tangu mwaka Agosti mwaka 2015 ambapo bei ya mafuta iliongezeka kwa Sh92 na kufanya lita moja ya petroli kuuzwa kwa Sh2290 huku dizeli ikiuzwa kwa Sh2026 kwa lita.

Kwa jiji la Dar lita moja ya petroli itauzwa kwa Sh2409 huku Dizeli ikiuzwa Sh2329.

Hali inaonekana kuwa mbaya zaidi katika mikoa ya Kagera, Geita, Tabora, Songwe, Iringa,Dodoma na Pwani ambapo lita moja ya petroli itauzwa (Sh2,624, Sh2,574, Sh2,563, Sh2,525, Sh2,473, Sh2,467 na Sh2,413) kwa mfuatano.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Ewura hakutakuwa na ongezeko la bei ya mafuta kwa mikoa ya kaskazini ikihusisha Tanga, Arusha na Kilimanjaro kutokana na bandari ya Tanga kutoingiza shehena mpya ya mafuta hivyo bei zitabaki zile zile za Juni.

Upande wa mafuta ya taa nako bei zitabaki kama ilivyokuwa mwezi uliopita kwa kuwa hakuna shehena mpya ya mafuta iliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Dar kwa mwezi Juni.

Na Elizabeth Edward, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527