WANANCHI WACHOMA MOTO MSITU WA MWEKEZAJI...DC NDAGALA APONGEZA

Wananchi wa kijiji cha Kiniha kata ya Mgunzu wilayani Kakonko mkoani Kigoma wameteteketeza msitu wa Mwekezaji uliokuwa karibu na shule ya msingi Kiniha baada ya msitu huo kuwa kero na kusababisha kifo kwa mwanafunzi mmoja na baadhi ya walimu na wanafunzi kutishiwa kubakwa katika msitu huo.


Hayo yamebainika jana katika ziara ya mkuu wa wilaya ya Kakonko alipotembelea Kata ya Mgunzu kusikiliza kero za wananchi na kuhimiza masuala ya maendeleo kwa wananchi ambapo mmiliki wa shamba hilo la miti Simon Matulane alitoa malalamiko kwamba serikali ya kijiji kwa kushirikiana na wananchi wamevamia shamba lake la msitu na kuliteketeza hivyo kusababisha afirisike.


Akielezea kuhusu uamuzi huo uliofikiwa na wananchi pamoja na serikali ya kijiji, Mwenyekiti wa kijiji cha Kiniha Isaya Mpamo  alisema baada ya kutokea tukio la kubakwa kwa mtoto na kuchinjwa wao kama serikali ya kijiji waliamua kumuita mwekezaji wa eneo hilo na kumuomba afyeke baadhi ya miti ya asili ili kuondoa kero kwa wakazi wa kijijini hapo ambapo msitu huo ulikuwa tishio kwa wananchi, walimu na wanafanzi kukimbizwa na wavuta bangi na lakini pia wanafunzi kujificha katika Eneo hilo na kushindwa kuhudhuria masomo.

Alisema waliitisha mkutano wa kijiji na kumpa muda aweze kufyeka miti ya asili na miti iliyopandwa iweze kutengenezwa vizuri lakini mwekezaji huyo alikaidi maamuzi ya mkutano mkuu na   baada ya kushindwa kufanya hivyo walifikisha barua na Mihutasari kwa katibu tawala wa wilaya na kuwaagiza waende kwa afisa wa misitu kufuata sheria baada ya hapo walipewa kibali cha kufyeka miti yote ya asili na kumuachia miti aliyopanda ili kutatua kero hiyo.

"Eneo hili lilikuwa kero sana limewatesa sana wananchi wa kijiji hiki na tuliumia baaada ya kuona mtoto wetu amefariki kwa kubakwa na mwalimu mwingine alinusurika , wanafunzi wamekuwa wakiingia katika msitu huo wanajificha na walimu hawawaoni hivyo kupelekea utoro kwa wanafunzi kuongezeka", alisema mwenyekiti wa kijiji. 

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walisema msitu huo ulikuwa kero kwao na wanafunzi wengi walikuwa wakiogopa kwenda shuleni kutokana na kuhofia kubakwa au kuchinjwa baada ya msitu huo kuteketezwa eneo hilo limekuwa shwari na wanafunzi wanaendelea na masomo vizuri.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala alisema hatua iliyochukuliwa na kijiji imezingatia haki na kumtaka mwekezaji huyo kuvuna hiyo miti iliyobaki na kutoa wito kwa wananchi wote wanaohitaji kuvuna miti yao kuomba kibali cha uvunaji kutoka serikalini kwa kuwa ni sheria ya misitu inasema hivyo.


Aidha aliwaasa wananchi kuendelea kulinda mazingira na kuwataka wenyeviti wa vijiji kuunda sheria ndogo ndogo za kuzuia uchomaji wa misitu na uharibifu wa mazingira na kuwaahidi wananchi na wenyeviti wa kijiji kwamba eneo litakalokutwa limechoma hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wananchi na viongozi wao wa kijiji.

"Kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa mazingira hasa kwa kipindi hiki cha kiangazi, watu mmekuwa mkishindishana kuchoma moto maeneo yenu niwaombe tabia hiyo iishe maana mnaendelea kusababisha matatizo makubwa, itafikia kipindi tutakosa mvua kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi jambo ambalo ni hatari kwa vizazi vijavyo", alisema Kanali Ndagala.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiniha kata ya Mgunzu wilayani Kakonko mkoani Kigoma. Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527