MUME AMTEKETEZA KWA MOTO MKEWE....WANAFUNZI WACHOMANA VISU


Watu watatu wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti wakiwamo mume na mkewe kuteketea ndani ya nyumba eneo la Mailimoja, Kibaha.


Katika tukio la Kibaha, Hussein Zaidi (58) anadaiwa kumfungia ndani ya nyumba mke wake mdogo, Zainab Juma (42) kisha kuichoma moto nyumba hiyo.


Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Jonathan Shanna alisema Hussein alijaribu kujiua akiwa amejifungia ndani ya nyumba yake pamoja na mkewe kwa kuzikusanya nguo na kuziwasha moto.


“Kabla ya kutekeleza tukio hilo kwanza alijaribu kumchoma mke wake huyo kwa kisu, alipoona hajafanikiwa aliamua kuichoma moto nyumba wote wawili wakiwa ndani,” alisema Shanna.


Alisema baadhi ya majirani walifika kutoa msaada baada ya kuona nyumba inawaka moto na kuwajulisha polisi waliofika eneo hilo.


Katika tukio jingine, mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Azimio Wilaya ya Tarime mkoani Mara mwenye miaka 15, anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kumchoma kisu na kumuua mwanafunzi mwenzake, Rhobi Chacha (14).


Kamanda wa polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema tukio hilo lilitokea juzi na Rhobi alifariki dunia saa sita mchana wakati akipata matibabu Hospitali ya Mji wa Tarime.


Marehemu alikuwa mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Azimio na mkazi wa Iganana, kata ya Sabasaba, Tarime.


“Baada ya kitendo hicho mtuhumiwa alikimbia na polisi tunamtafuta ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Mwaibambe.


Kaimu mganga mkuu wa Hospitali ya Mji Tarime, Dk Innocent Kweka alisema alimpokea Rhobi juzi saa nne asubuhi lakini alifariki dunia akiendelea na matibabu.


“Kwenye uchunguzi ilibainika kuwa alichomwa na kitu chenye incha kali na kilizama kwenye mapafu, hali iliyosababisha marehemu kuvuja damu na kupoteza maisha,” alisema Dk Kweka.


Akizungumzia tukio hilo mwalimu mkuu msaidizi shuleni hapo, Bahati Lucas alisema Rhobi na Charles wanasoma shuleni hapo. “Inasikitisha sana, mtuhumiwa alikuwa anatarajia kufanya mtihani wake wa mwisho wa darasa la saba mwaka huu,” alisema.


Naye mwenyekiti wa mtaa wa Iganana, Edward Thomas alisema mtuhumiwa na Rhobi ni majirani wanaotenganishwa na barabara ya mtaa. “Ulizuka ugomvi kati yao wakati wanacheza mpira, mtuhumiwa aliingia nyumbani na kuchukua kisu na kumshambulia mwenzake,” alisema Thomas.

Na Julieth Ngarabali na Waitara Meng’anyi, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527