Friday, June 29, 2018

MSHITAKIWA AMTANDIKA NGUMI ZA KUTOSHA MSIKILIZAJI MAHAKAMANI ARUSHA

  Malunde       Friday, June 29, 2018


Mmoja kati ya washitakiwa wanne wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya Mchungaji Nixon Isangya (71), amezua kioja mahakamani baada ya kumshambulia kwa ngumi mmoja ya wasikilizaji katika chumba cha Mahakama.


Washitakiwa hao wakiwa mbele ya Hakimu Nestory Baro wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, walizua tafrani hiyo baada ya mshitakiwa Obadia Nanyaro (60) ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa Kanisa la International Evangelism, kumpiga msikilizaji, Agustino Nko baada ya kesi hiyo kuitwa mahakamani hapo.

Tukio hilo lisilo la kawaida, liliwaacha vinywa wazi watu waliokuwepo mahakamani, hapo akiwemo Hakimu huyo na wanasheria kadhaa.

Baada ya kesi hiyo kuitwa mbele ya Hakimu Baro, mmoja ya wasikilizaji alitangulia ndani ya chumba cha Mahakama na kujibanza mahali, kwa lengo la kuwaona washtakiwa vizuri.

Washitakiwa walipofikishwa katika chumba hicho na kuingia ndani, ndipo mshitakiwa huyo alipomkunja msikilizaji huyo na kumpiga ngumi za kutosha, kabla ya askari waliokuwa wameambatana nao kuamua ugomvi huo.

Sababu za kitendo hicho hakijajulikana, ila inadaiwa wahusika wamekuwa na uhusiano mbaya kwa muda mrefu baina yao na kwamba kitendo cha kukutana eneo hilo, kiliibua hasira kwa mshitakiwa.

Hata hivyo, Hakimu Baro aliamuru mtu huyo aliyeshambuliwa apelekwe Mahabusu kwa nusu saa kutokana tukio hilo la kustaajabisha, lililojitokeza mahakamani hapo.

Mahakama hiyo ilielezwa kwamba upelelezi wa shauri hilo, bado haujakamilika na hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 9, mwaka huu.

Washitakiwa wengine ni Ndewario Nderekwa (59), ambaye ni mdogo wa marehemu Isangya, Joshua Pallangyo (42) na Simoni Kaaya (42) wote wakazi wa Sakila, Arumeru mkoani Arusha.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Penina Joackim aliiambia mahakama hiyo kwamba Aprili 7, mwaka 2017 katika eneo la Moivaro ndani ya Jiji la Arusha, washitakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa kwa kumuua Isangya ambaye alikuwa ni mkazi wa eneo la Sakila Chini Kikatiti.
Chanzo- Habarileo
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post