BOSI WA MABASI YA ZACHARIA ANASHIKILIWA KWA KUWAJERUHI KWA RISASI MAAFISA USALAMA WA TAIFA


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima. 

 Unaweza kusema taarifa za kutoweka kwa mfanyabiashara maarufu na kada wa CCM wilayani Tarime, Peter Zakaria zimetolewa ufafanuzi.


Leo Jumamosi Juni 30, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ametoa ufafanuzi kuhusu tajiri huyo ambaye ni mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Zakaria kuwa hajatwekwa.


Akizungumza na waandishi wa habari Malima amesema mfanyabiashara huyo amekamatwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na kufikishwa kituo cha polisi mjini Tarime kwa ajili ya kuhojiwa, akituhumiwa kuwajeruhi kwa risasi maofisa wawili wa idara hiyo.


Amesema kabla ya tukio hilo, maofisa watano wa Usalama wa Taifa walifika katika kituo cha mafuta kinachomilikiwa na Zakaria kwa nia kujaza mafuta kwenye gari lao, “ wenzao wawili walishuka kwenye gari ghafla wakashambuliwa kwa risasi na Zakaria aliyekuwepo eneo hilo.”


"Baada ya wenzao kujeruhiwa kwa risasi, maofisa wengine walifanikiwa kumdhibiti Zakaria na kumtia mbaroni na kumkabidhi kwa polisi wanaoendelea kumhoji.”


Malima hakutaka kulizungumzia kwa undani tukio hilo lililotokea jana Juni 29, 2019 saa 2:30 usiku na kubainisha kuwa waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Tarime huku mmoja akidaiwa kuwa katika hali mbaya.


Tangu jana usiku, mji wa Tarime umekumbwa na taharuki baada ya taarifa za mfanyabiashara huyo kudaiwa kutekwa kuzagaa mitaani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527