Monday, June 18, 2018

KUONDOA VAT TAULO ZA KIKE TABASAMU KWA MWANAMKE

  Malunde       Monday, June 18, 2018

Pendekezo la Serikali la kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa taulo za kike za usafi linaweza kumpa tabasamu mwanamke si kijamii pekee, bali pia kiuchumi.


Akiwasilisha bungeni Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali inakusudia kuondoa Vat kwa bidhaa hiyo.


Litakapopitishwa na Bunge, pendekezo hilo litamwezesha mwanamke kuokoa zaidi ya Sh7,000 kwa mwaka.


Kwa kufuta kodi hiyo, gharama za bidhaa hiyo itapungua kwa wastani wa asilimia 15 kulingana na aina na bei ya bidhaa husika.


Tathmini iliyofanywa na mwandishi wetu inaonyesha kwa wastani mwanamke hutumia zaidi ya Sh36,000 kwa mwaka kwa ajili ya kununua taulo hizo na kutokana na kuondolewa Vat gharama inatarajiwa kupungua hadi kufikia Sh29,232.


Hesabu imefanywa kwa kuzingatia kiwango cha taulo 144 anazoweza kutumia mwanamke kwa mwaka iwapo atatumia taulo mbili hadi tatu kwa siku, katika kipindi cha siku nne kwa mwezi.


Bei iliyotumika ni ya wastani wa Sh2,000 kwa rejareja kwa pakiti moja yenye taulo nane.


Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi alisema kina mama na wasichana hutumia gharama kubwa kununua bidhaa hiyo, hivyo kuondolewa Vat kutawezesha wazalishaji na wasambazaji kushusha bei.


“Wazalishaji wengi wamekuwa wakilalamikia kodi ya Vat na hasa kwa kuzingatia kuwa wengi wanaagiza kutoka China. Kutokana na hatua hii ya Serikali tunapanga kukutana na wazalishaji,” alisema.


Alisema kwa kuonana na wazalishaji, wataangalia kiasi cha bei kitakachotakiwa kupunguzwa.


Rebeca alisema punguzo hilo si haba kwa kuzingatia kuwa ni kilio cha muda mrefu kwa watumiaji wengi.


Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza alisema jana kuwa hatua hiyo ya Serikali inapaswa kupongeza licha ya kwamba punguzo ni dogo.


Alisema Serikali inapaswa kuanza kufanya uchunguzi ili kujiridhisha na mwenendo wa bidhaa hiyo na kubaini mtumiaji atalazimika kutoa kiasi gani cha fedha hadi inamfikia mkononi mwake.


“Tunataka bei iwe rafiki ili kila mtu aweze kuimudu. Nimefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Serikali kuanza kuyafanyia kazi mahitaji yetu,” alisema Upendo.


Mbunge huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigania usambazaji bure wa bidhaa hiyo katika shule za msingi na sekondari, alisema Serikali pia ingeanza kutoa ruzuku kwa mmoja wa wasambazaji kama ilivyo kwa kondomu.
Na George Njogopa, Mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post