Saturday, June 23, 2018

MKUTANO WAZIRI MKUU WAPIGWA BOMU....WATU KADHAA WAMEKUFA

  Malunde       Saturday, June 23, 2018

 Mlipuko mkubwa ulitokea katika mkutano  leo Jumamosi Juni 23, 2018 ambao waziri mkuu mwanamageuzi Dk Abiy Ahmed alikuwa akihutubia kwenye uwanja wa Meskel katikati ya jiji na baadaye aliliarifu taifa kwamba watu kadhaa wamekufa.

Akilihutubia taifa muda mfupi baada ya mlipuko huo, Abiy alisema “watu kadhaa” walikufa kutokana na mlipuko huo na alitoa salamu za rambirambi kwa familia zilizofiwa na jamaa zao.

Abiy alikuwa amemaliza kuhutubia na alikuwa akiwapungia mikono maelfu ya wafuasi wake waliohudhuria mkutano huo ndipo ukatokea mlipuko huo.

Waziri mkuu hakujeruhiwa na aliondolewa kwa haraka na maofisa wa usalama kutoka eneo hilo.

Mwandaaji wa mkutano huo, Seyoum Teshome alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook kwamba "Waziri Mkuu Abiy na wageni wengine waliohudhuria mkutano huo ni wazima."

Shirika la utangazaji ambalo lilikuwa linatangaza shughuli za mkutano huo ghafla lilisitisha matangazo na mara wakawa wanasikika watu wakiimba, wakipiga mayowe wakirejea majumbani kwao.

Magari ya kubeba wagonjwa yalionekana katika eneo la Meskel Square ambako waziri mkuu alikuwa akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake.

Umati mkubwa wa watu ulikusanyika katika mkutano huo ulioandliwa kuiunga mkono serikali ya kiongozi huyo mpya anayeidhinisha mageuzi ambayo hayajawahi kushuhudiwa nchini.


Mashuhuda wasema

Haikujulikana idadi ya watu walioathirika lakini ilibidi kiongozi huyo aondoshwe kwa haraka chini ya ulinzi muda mfupi baada ya kutoa hotuba yake.

Maelfu walikuwa wamekusanyika katika bustani kuu ya Meskel mjini Addis Ababa. Vyombo vya habari nchini viliripoti kwamba watu kadhaa walijeruhiwa na walipelekwa katika kituo cha afya kilicho karibu na bustani hiyo kupatiwa matibabu.

Mwandishi wa shirika la habari la AP aliwaona makumi ya watu wakiwa wamejeruhiwa katika mkutano huo wa Jumamoso. Picha za video zilimwonyesha Abiy akiondolewa eneo la tukio ka haraka na walinzi wa usalama.

Aidha, mwandishi wa BBC aliyekuwa katika eneo hilo alisema kulikuwa na kelele nzito na kubwa iliyosikika karibu na jukwaa walipokaa watu mashuhuri muda mfupi baada ya waziri mkuu kumaliza kuuhutubia umati.

Abiy mwenye umri wa miaka 42 aliingia madarakani Aprili na haraka alianza kuwashangaza watu wengine katika taifa hilo la pili Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu alipoamua kufanya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.

Akiwa amevaa fulana, Abiy alihutubia idadi kubwa ya watu ambao hawajawahi kuonekana katika miaka ya hivi karibuni waliokuwa wamevaa mavazi yenye picha ya waziri mkuu huyo na maandishi yasemayo "One Love, One Ethiopia".

Hali ya utulivu sasa imerejea na polisi wanasema wanachunguza tukio hilo.
 Chanzo- Mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post