WATAALAMU KUTOKA HALMASHAURI SITA WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO RAHISI WA UPIMAJI ARDHI

Wataalamu 16 kuoka Halmashauri za Wilaya ya Morogoro, Mvomero, Bahi, Kongwa, Kilolo na Mufindi walio chini ya Idara ya Ardhi, maliasili na mazingira wamejengewa uwezo juu ya utumiaji wa mfumo mpya na rahisi wa upimaji ardhi unaofahamika kwa jina la MAST (Mobile Application for secure tenure).

Akiongea Mkoani Iringa wakati wa ufunguzi wa ziara hiyo ya mafunzo iliyoandaliwa na Shirika la PELUM Tanzania, Donati Senzia Mratibu wa PELUM alisema lengo hasa la ziara hiyo ni kuwapatia elimu wataalamu hao na kuona ni jinsi gani wataweza kuutumia mfumo huo kwenye Halmashauri zao kupitia miradi ya upimaji ardhi ambayo watakuwa nayo. 

Akifafanua jinsi mfumo huo unavyofanya kazi, Mustapha Issa ambaye ni Mkurugenzi msimamizi wa shughuli za miradi USAID LTA-Iringa, alisema kuwa mfumo huu ulitengenezwa kwa ajili ya uhakiki wa maslahi na upimaji wa vipande vya ardhi ambao hutumia simu za kisasa. 

Alisema mbali na kuwa mfumo huu kutoa ajira kwa vijana wengi kama wapimaji wasaidizi baada ya kupatiwa mafunzo jinsi ya kuutumia lakini pia mfumo huu ni rahisi na hautumii muda mwingi kuanzia kwenye zoezi la upimaji, uchukuaji taarifa, utunzaji taarifa hadi kufikia hatua ya kutoa hatimiliki. 

Halikadhalika mchoro unajichora wenyewe moja kwa moja wakati wa upimaji kipande, upigaji wa picha hufanyika na kuhifadhiwa kwenye mfumo mara tu baada ya mpimaji kujiridhisha na taarifa ya mteja wake na wakati huohuo taariza zote za mmiliki wa kipande husika zinachukuliwa na kuhifadhiwa na mfumo kwa ajili ya kukamilisha zoezi la utoaji wa hatimiliki. 

Akielezea utofauti alioubaini kwenye kipimo hiki cha MAST, Fred Mgeni Afisa Mipango miji na vijiji Halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Iringa anasema mbali na mfumo huu wa MAST kuchora mchoro wa kipande kilichopimwa (umbo) moja kwa moja tofauti na kipimo kinachotumika sasa, tofauti nyingine iliyopo ni kuwa kipimo cha sasa kina mapungufu ya uhakiki kuanzia mita 1-10 jambo ambalo halitakiwi na inashauriwa walau mapungufu hayo yasizidi mita 1-3. 

“Kupitia ziara hii ya mafunzo nimegundua sisi kama PELUM Tanzania tungeweza kupima zaidi ya vijiji 28 na kuvuka lengo la mradi na kugawa hatimiliki mapema zaidi kwa kila kijiji tunachomaliza kupima kwani kwa kupitia mfumo huu, jumla ya hatimiliki 200 hudurufiwa kwa siku kwa kuwa kila taarifa inakuwa ndani ya mfumo hakuna uhamishaji wa taarifa mara mbilimbili na zitatunzwa kwa ufasaha zaidi”. Angolile Rayson Afisa Mradi toka PELUM Tanzania. 

Naye Bernard Kajembe Afisa Mipango Miji na vijiji Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Iringa anasema, pamoja na kuwa mfumo wa MAST kuwa rahisi wakati wa utekelezaji wa shughuli za upimaji vipande, uingizaji wa taarifa hadi uandaaji wa hatimiliki lakini pia ananashauri kuwa, 

“Ni vyema kuhakikisha kila mtaalamu toka Halmashauri husika anayehusika kwenye zoezi la upimaji wa vipande vya ardhi awe anahakiki taarifa zake muhimu kabla ya kutoa hatimiliki ili kusiwepo muingiliano wa taarifa ambazo zinaweza kuchangia kutokea kwa migogoro ya ardhi kati ya wanawanachi wenyewe ama wananchi na serikali kwa kutumia maeneo yaliyetengwa na Serikali kwa matumizi mengine”. 

Georgina Kallaghe afisa ardhi toka Wilaya ya Bahi anasema, mbali na mfumo huu kurahisisha upachikaji wa picha ya muhusika moja kwa moja kwenye taarifa zake tofauti na mfumo wa sasa ambao unaleta mvurugano kutambua picha sahihi ya muhusika na hasa zikikaa muda mrefu na wakati mwingine kuchangia fomu zilizojazwa taarifa za mteja kupotea ama kuliwa na panya pindi wanaporudishiwa kufanya uhakiki wa taarifa zao muhimu 

Lakini pia anasema mfumo huu unaweza kutumiwa na mtu yeyote yule na hasa upande wa uchukuaji jira kwani mchoro hujichora wenyewe tofauti na ilivyo sasa hadi umsubiri ama kumtafuta Afisa mipango miji ama mpima ardhi achore mchoro husika 

Kwa upande wake Andrea Biashara afisa mipango miji na vijiji Halmashauri ya Morogoro amesema, utofauti aliouona ambao nao pia unatumia gharama ndogo ni kudurufu hatimiliki kwa kutoa picha ya muhisika bila rangi jambo ambalo ameshauriana na kamishina wa ardhi wa vijiji pamoja na wataalamu wengine toka Wizarani ili kuendelea kufanya hivyo kama sehemu ya kuwezesha hati nyingi kutolewa kwani gharama ya wino wa rangi kwa mashine kubwa inayotoa hati nyingi inafika hadi milioni sita jambo ambalo halmashauri nyingi haziwezi kulileba. 

Mbali na kufanikiwa kutengeneza hatimiliki 40,000 kwenye vijiji 28 vya mradi ndani ya miaka miwili, Mustapha Issa ambaye ni Mkurugenzi msimamizi wa shughuli za miradi USAID LTA-Iringa alisema lengo lao kuu ni kuhakikisha mfumo huu unatumika nchi nzima kwani wameshatoa elimu hii kwenye Halmashauri nane nchini, Wizara ya ardhi maendeleo na mkazi, Tume ya Taifa ya usimamizi wa mipango ya matumizi bora ya ardhi, Chuo kikuu cha ardhi pamoja na mashirika binasfi manne. 
Mustapha Issa Mkurugenzi msimamizi wa shughuli za miradi USAID LTA-Iringa, akielezea jinsi mfumo wa MAST unaotumia simu za kisasa unavyofanya kazi wakati wa upimaji wa vipande vya ardhi.
Sadoth Kyaruzi Afisa Mpango miji na vijiji halmashauri ya Mvomero, Morogoro akichangia jambo wakati wa mafunzo ya MAST.
Timu ya wataalamu kutoka Halmashauri za wilaya sita, Morogoro, Mvomero, Kilolo, Mufindi, Bahi na Kongwa. Wawakilishi toka masharika wanachama (INADES na UMADEP) pamoja na maafisa mradi wa PELUM Tanzania wakipewa maelezo na mmoja wa vijana waliopewa mafunzo juu ya utumiaji wa mfumo wa MAST.
Timu ikichukua alama za shamba la mwananchi (wakiongozwa na mmiliki wa shamba) ili kuweza kupata mchoro kamili na ukubwa wa shamba husika
Timu ikikagua mchoro wa shamba husika kupitia mipaka/alama walizokuwa wakionyeshwa na mwenye shamba
Mmoja wa washiriki baada ya kukagua taarifa za wateja akihoji kutaka kufahamu nini hufanyika baada ya kukuta taarifa ya mteja imekosewa na hasa kama mtu alipima eneo lisilo lake ama lina mgogoro wa ardhi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527