Picha: VIJANA 798 WAHITIMU MAFUNZO YA JKT KAMBI YA MTABILA KIGOMA, DC ATAKA WARUDI VIJIJINI KUMALIZA UMASKINI

Vijana waliopitia Mafunzo ya awali ya jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wametakiwa kurejea vijijini na kushirikiana na Halmashauri kuanzisha miradi mbalimbali na kuhakikisha wanawaelimisha Vijana wengine kuondokana na umaskini kwa kutumia mafunzo waliyoyapata wakati wa kozi hiyo.

Wito huo umetolewa leo  na Mkuu wa wilaya ya Buhigwe na kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Brigedia Jenerali Marco Gaguti Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, wakati akifunga mafunzo ya awali kwa Vijana 798 wa oparesheni mererani waliohitimu mafunzo yao ya awali katika kambi ya Mtabila, ambapo aliwataka vijana hao kuondokana na Mawazo ya vijana wasomi ya kutaka kuajiriwa na kuyatumia mafunzo waliyoyapata kuanzisha miradi mbali mbali na kujiajiri na kuwaelimisha vijana walioko mtaani.

Jenerali Gaguti aliwataka vijana wote waliohitimu mafunzo ya oparesheni Magufuli na oparasheni zingine kurudi katika wilaya ya Kasulu na Buhigwe kuanzisha vikundi vya ujasiriamali kutumia mafunzo waliyoyapata na kushirikiana na vijana walioko mtaani kuhakikisha fedha zinazotolewa na Halmashauri kwa ajili ya mfuko wa vijana kutumika kuondoa umaskini .

"Nitoe Wito kupitia hadhara hii kwa vijana wote ambao ni wa Buhigwe na Kasulu na wilaya nyingine za mkoa wa Kigoma mrudi vijijini washirikiane na vijana wengine waliopo mtaani, sifurahishwi na vijana wanaolalamika kuwa hakuna ajira lazima mshirikiane kuhakikisha tunaondokana na kundi kubwa la vijana wanaodai hakuna ajira", alisema Jenerali Gaguti.

Aidha alisema kuhusiana na suala la kukosekana umeme katika Kambi hiyo kulicheleweshwa na migogoro iliyokuwepo baina ya wakandarasi wa Umeme wa REA awamu ya tatu ambapo mgogoro huo umemalizika na mwezi Juni mwaka huu wataanza kusambaza umeme wa REA kwa wilaya ya Kasulu na kuwaahidi kuanza kuweka nguzo ya kwanza katika eneo la kambi hiyo.

Akimkaribisha Mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Kambi ya Mtabila Meja Peter Lyanga alisema wanafunzi walioanza mafunzo ya awali ya oparesheni Mererani walikuwa wanafunzi 806 na waliohitimu ni vijana 798 na vijana nane wameshindwa kumaliza Mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa na utoro.

Alisema mafunzo waliyoyapata Vijana hao yamewajenga kuwa wazalendo na kujitegemea pindi wawapo uraiani na kuwaomba vijana hao kuendelea kuyaishi mafunzo waliyojifunza na kuhakikisha kiapo chao lakini pia wawe vijana bora kule ndani JKT katika kipindi cha miezi 18 ya mafunzo ya stadi, kwa wale ambao hawatapata nafasi ya ajira wasikate tamaa kwani jkt limewapa stadi za maisha kutosheleza kujiajiri na kuongoza wengine.

Aidha aliwataka kuwa tayari kulilinda taifa la Tanzania pindi wakihitajika.

Wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi wahitimu hao Rosemary Lyimo alisema mafanikio waliyoyapata ni kuwa na ukakamavu na kwa kujifunza kuwa na umoja bila kujali udini na ukabila pamoja na shughuli za uzalishaji mali ambapo wameanza kufanya kazi pamoja na kujenga nyumba ya mkuu wa kikosi hicho.

Alisema pamoja na mafanikio hayo changamoto zilizojitokeza ni ukosefu wa umeme katika Kikosi na kikosi kina uhitaji wa mwanga katika kuimarisha ulinzi na usalama, muingiliano wa Barabara baina ya kambi na wanakijiji na kuomba Changamoto hizo zitatuliwe ilikuweza kuiweka kambi salama.
Na Rhoda Ezekiel- Malunde1 blog

ANGALIA PICHA 
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Brigedia Jenerali Marco Gaguti akikagua gwaride - Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527