Friday, May 18, 2018

WAKULIMA WA PAMBA KIGOMA WAPEWA TAHADHARI

  Malunde       Friday, May 18, 2018
Wakulima wa zao la pamba wilayani Kakonko mkoani Kigoma wametakiwa kuwaepuka wanunuzi wa pamba ambao hawatambuliki kisheria ili kuepukana na usumbufu wakati wa kuuza pamba zao.


Kauli hiyo imetolewa jana katika Kijiji cha Kanyonza Wilaya ya Kakonko, na afisa kilimo wa Mkoa wa Kigoma Joseph Lubuye wakati wa Uzinduzi wa uuzwaji wa zao la pamba mkoa wa Kigoma uzinduzi uliofanyika katika kata ya Kanyonza ambayo inaongoza kwa kilimo hicho Mkoani Kigoma.

Lubuye aliwataka wakulima hao kuuza pamba hiyo katika vikundi vya ushirika na kampuni iliyopewa dhamana na serikali ya kununua zao hilo.

Lubuye alisema Kampuni itakayo husika na uuzaji na manunuzi ya pamba ni kampuni ya Kahama Cotton Campany Limited(KCCL) ambayo itashirikiana na chama cha ushirika lengo ikiwa ni kuhakikisha mkulima haibiwi na pamba inayo uzwa na kununuliwa ni yenye ubora wa hali ya juu na kuepusha migogoro.

Alisema kwa mwaka huu pamba itauzwa kwa shilingi 1,100 kwa kilo na kuwaomba wakulima kutumia nguo katika kubebea pamba na kuwaasa kuwa mkulima yeyote atakae weka mchanga au maji kwenye pamba ilikuongeza uzito ataadhibiwa, na kuwaomba wakulima kuwa wavumilivu kwakuwa mwakani watapatiwa pembejeo za kilimo bure na viuwatilifu.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga aliwataka maafisa kilimo wote kuhamia vijijini kwa msimu huu wa uuzwaji wa pamba na kwamba msimu wote wa kilimo maafisa kilimo wote wanatakiwa kuondoka mjini na kuhamia vijijini kuwafundisha wakulima kulima mazao yenye ubora na kwa kufuata maelekezo ya wakulima na kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Kigoma kuepukana na umaskini.

"Niwaagize maafisa kilimo msimu wote huu wa uuzwaji wa pamba mje huku kukaa na wananchi mtoe maelekezo watakachokula wananchi na nyie mtakula hicho hicho kwa kuwa wananchi hawa ndiyo waajili wetu, Mkoa wa Kigoma hatuhitaji matabaka ya watu ya wenye nacho na wasio nacho lazima tuhakikishe tunaunga mkono juhudi za wananchi kuweza kuinua uchumi wa wananchi na kipato kwa wakulima", alisema Maganga.

Aidha mkuu huyo aliwaomba wakulima kuendelea kuwa wavumilivu na kukabiliana na bei iliyopangwa , kwa kuwa serikali imepanga kuwasaidia kwa kuwapa viuwatilifu na pembejeo bure na kutoa wito kwa wasambazaji wa mbegu kuhakikisha wanaleta mbegu za kisasa kwa msimu ujao ilikuweza kuwatia moyo wakulima kuendelea kulima zao hilo.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa katika uzinduzi wa uuzwaji wa zao hilo Mkuu wa Wilaya ya Kakonko ,Kanali Hosea Ndagala alisema ukizungumzia kilimo cha pamba Mkoani Kigoma lazima uizungumzie Kakonko kwa kuwa ndiyo wilaya iliyo na wakulima wengi na wamejipanga kuongeza wakulima zaidi msimu ujao kwa kuhahikisha wakulima wanapata pembejeo za kutosha.

Alisema kwa msimu huu waliwashawishi wakulima na wakulima waliongezeka kutoka wakulima 247 kwa msimu wa mwaka 2016/2017 na kufikia wakulima 1307 kwa mwaka 2017/2018 na zaidi ya hekta 1800 zimelimwa na matarajio ni kuhakikisha kwa mwaka huu wanapata zaidi ya tani 1159.6 kutokana idadi ya wakulima na hali ya pamba ilivyo shambani.

Nae Katibu wa Chama cha ushirika cha msingi Kakonko, Boniventura Sylivester alisema changamoto waliyo kutana nayo kwa Mwaka huu ni kuletewa dawa ambazo haziuwi wadudu hali inayopelekea pamba kuhalibika na kuomba serikali kuwahimiza wasambazaji wa dawa kutengeneza dawa za mafuta zinazo uwa wadufu haraka na kuacha kuwaletea dawa za maji.

Hata hivyo waliiomba serikali kuwasaidia wakulima katika suala la bei kwakuwa msimu uliopita bei ilikuwa ni 1,200 kwa sasa bei imeshuka hali inayo wakatisha tamaa wakulima na kuomba bei iongezwa ilikuweza kuwatia moyo wakulima kwakuwa walitumia gharama kubwa kwaajili ya viuwatilifu na mbegu.

Na Rhoda Ezekiel- Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga akizungumza


Mkuu wa Wilaya ya Kakonko ,Kanali Hosea Ndagala akizungumzaUsikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post