VIBAO VYA SPIDI 50 BARABARA KUU DAR - MOSHI VYANG'OLEWA

Ni hatari kwa wakazi wa maeneo yaliyo pembeni mwa barabara ya Dar-Moshi; wananchi wameng’oa vibao vya alama za barabarani ambavyo ni maalumu kwa ajili ya kudhibiti mwendo wa magari na kuashiria vitu vilivyo mbele.


Eneo la zaidi ya kilomita 100 halina vibao hivyo na uchunguzi wa waandishi wetu unaonyesha vimeng’olewa na watu wasiotaka kudhibitiwa mwendo na hatimnaye kutozwa faini.


Uchunguzi huo uliothibitishwa na mamlaka za Serikali, umebaini vibao vilivyong’olewa au kufutwa alama katika eneo linaloanzia Wilaya ya Same hadi Moshi mjini, hasa vile vinavyotaka madereva kwenda mwendo wa kasi ya 50 kwa kilomita.


Inadaiwa njama za kung’oa au kufuta vibao hivyo vinavyokadiriwa kufikia 30 inaweza kuwa njia ya kukwepa faini za askari wa usalama barabarani, faini ambazo ni Sh30,000 kwa kosa moja.


Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, pale kibao kinapoonyesha ukomo wa spidi 30 kwa kilomita au 50, magari hayaruhusiwi kwenda zaidi ya mwendo huo na madereva wanaokiuka hutozwa faini hiyo.


Kuondolewa kwa vibao hivyo kunaweka rehani maisha ya abiria na watu wa vijiji vilivyo kando ya barabara hiyo ambao walishazoea kuvuka kwenye maeneo salama.


Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa Kilimanjaro na Arusha (Akiboa), Hussein Mrindoko alisema wana taarifa za kung’olewa kwa alama hizo.


“Vibao havipo barabarani kuanzia Same hadi Moshi na hatujui ni kwa nini,” alisema.


Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Zauda Mohamed alisema wanawasaka walioving’oa.


“Kuna baadhi ya alama za barabarani zimekuwa zikifutwa kwa kutumia spray (rangi). Hii inasababisha watumiaji wa barabara kukosa mawasiliano na alama nyingi zinazofutwa ni zile zinazoelekeza spidi,” alisema Zauda.


“Hili liko zaidi Moshi mjini na Mwanga. Limewaletea shida watumiaji wa barabara na kusababisha ajali hasa usiku. Mahali pengine vinafutwa vibao muhimu vya maelekezo ya vivuko na kona.”


Alisema inaonekana kuna kikundi cha watu wenye nia ovu wanaofuta na kung’oa alama hizo ili kuhalalisha kuvunja sheria.


Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nkolante Ntije alisema hawajawajua wahusika na wanafanya tathmini kujua idadi halisi ya vibao vilivyofutwa au kung’olewa.
Na Daniel Mjema na Florah Temba mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527