SAUTI NDANI YA KONTENA YAZUA TAHARUKI BANDARINI

Mkazi wa Miembeni mjini Unguja, aliyetajwa kwa jina moja la Hassan amenusurika kifo baada ya kutolewa ndani ya kontena alikojifungia.


Msimamizi wa makontena katika Bandari ya Malindi, Ibrahim Abdallah akizungumza na MCL Digital leo Mei 13, 2018 amesema chanzo cha mtu huyo anayekadiriwa kuwa na miaka 30 kuingia kwenye kontena na kujifungia hakijajulikana.


Amesema wakiwa katika kazi zao eneo hilo saa moja asubuhi walisikia sauti ikitoka ndani ya kontena lililo juu ya jingine hivyo kuzua taharuki miongoni mwao.


Abdallah amesema sauti iliyosikika kutoka ndani ya kontena ilisema, “Nakufaaa.”


Amesema walipofika eneo hilo waliuliza, “wewe ni nani” na jibu walilopatiwa ni, “Hassan.”


"Baada ya kutaja jina tulifungua kontena ambalo alikuwa amelifunga na kumtoa akiwa na hali mbaya kiafya na tulimpeleka Hospitali ya Mnazi Mmoja ili kupatiwa huduma ya kwanza," amesema.


Kuli katika bandari hiyo, Mohamed Khamis Makame amesema ni mara ya kwanza kutokea tukio hilo eneo hilo, hivyo amesema wanapaswa kuwa makini katika ulinzi.
Na Haji Mtumwa, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527