MBUNGE WA CHADEMA AELEZA SABABU ZA KUMSIFIA RAIS MAGUFULI

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amemsifu Rais John Magufuli kwa kupeleka fedha za maendeleo katika halmashauri yake bila ya kubagua, lakini amesema video iliyosambaa mitandaoni haitoi picha halisi ya alichosema.


Video hiyo fupi inamuonyesha Mchungaji Msigwa akizungumza kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika Ikulu ya Iringa juzi na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wa kisiasa na kidini.


“Na Mheshimiwa Rais umekuwa ukisisitiza kwenye hotuba zako kwamba wewe hujali vyama na hili limedhihirika kwa kweli kwamba hujali vyama,” anasema Mchungaji Msigwa katika video hiyo huku waalikwa wakimpigia makofi.


“Umesaidia sana. Bahati mbaya hawakukupangia ratiba ya kufungua miradi. Hela za kutoka kwako zimekuja nyingi. Amezungumza Mheshimiwa (Waziri wa Mambo ya Nje, Augustine) Mahiga, tuna barabara nzuri.


“Katika kipindi chako ambacho umekuwa Rais tumejenga barabara ya lami ya mradi wa World Bank kutoka Mlandege mpaka kwa mkuu wa wilaya, karibu Sh3.5 bilioni, tuna stendi nzuri iko hapo chini Ipogolo, karibu Sh3 bilioni. Tuna maji. Kwa hiyo kuna vitu vimefanyika.


“Kwa kweli Mheshimiwa Rais hupendelei, hata sisi wa Chadema unaleta hela. Kwa hiyo wewe hujali vyama. Unaleta hela. Kwa hiyo wewe huwa hujali vyama hilo nikupongeze sana.”


Wakati akisema hayo, picha zinaonyesha waalikwa wakiangua vicheko na sauti zao zinasikika wakati akihitimisha hotuba yake.


Msigwa ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Serikali ya Awamu ya Tano na alipotafutwa kuelezea kwa kirefu alichokizungumza alisema, “Wamechukua kipande kidogo ambacho nilisema hela zimeletwa Manispaa ya Iringa, lakini wameacha kipande kikubwa ambacho nilizungumza kwamba hata kama madiwani wameondoka, Manispaa ya Iringa imekuwa nzuri, imekuwa bora,” alisema jana.


“(Wanachama wa Chadema na Ukawa) Wasione kama kuna mtu hapa ameyumba au nimesalimu amri. Mapambano bado yanaendelea, hiyo ndiyo hoja.”


Kuhusu alichokizungumza, alisema kauli yake ilimaanisha kuwa Manispaa ya Iringa imekuwa bora katika kipindi hiki ambacho imekuwa chini ya Chadema kwa kuwa Rais amekuwa akipeleka fedha bila ya kujali vyama, lakini akashangaa kwamba ratiba yake mkoani Iringa haikujumuisha kutembelea miradi mikubwa kama barabara, machinjio kubwa kuliko zote Tanzania, stendi na mambo mengine.


“Kuna miradi mingi imefanyika chini ya uongozi wetu ambayo haihusiani na uwepo wa CCM ambao wapo katika manispaa hii na kumekuwa na dhana kuwa watu wakiwa Chadema au kiongozi akiwa Chadema, hakuna maendeleo na ndio maana madiwani wamekuwa wakihama,” alisema.


“Kwa mfano, tuna barabara ambayo imejengwa kwa Sh3.5 bilioni na ambayo haikuwapo. Tumejenga katika kipindi hiki ambacho manispaa inaongozwa na Chadema.”


Pia alisema kuna machinjio ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, pamoja na stendi ya mabasi iliyokamilika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527