HII NDIYO MIKOA AMBAYO MAAMBUKIZI YA VVU YAMEPANDA


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameitaja mikoa ya Tanga,Mwanza na Dodoma kuwa ndiyo mikoa ambayo  kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kinazidi kupanda. 

Akizungumza leo Mei 9,2018 wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wa nne wa VVU na UKIMWI na sherehe za miaka 30 ya mpango wa taifa wa kudhibiti Ukimwi, katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo katika chuo cha Mipango jijini Dodoma,Waziri Ummy alisema ipo haja ya wadau wote kushirikiana katika kuhakikisha maambukizi yanapungua.


Amesema maambukizi yanazidi kuongezeka katika mikoa 11 nchini ukiwemo mkoa wa Dodoma, Tanga na Mwanza licha ya kiwango cha maambukizi kitaifa kushuka kutoka asilimia 7 mwaka 2003/04,hadi asilimia 4.7 kwa mwaka 2016/17.

"Wakati maambukizi ya VVU yakipungua kitaifa lakini katika mikoa 11 yamepanda mfano Tanga ilikuwa na maambukizi kwa asilimia 2.4% lakini sasa ni 5% ,Dodoma 2.9% sasa ni 5% na Mwanza 4.2% sasa imekuwa 7.2 %",alieleza.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile amesema mpaka sasa serikali haijapata tiba ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi licha ya kuanza majaribio ya dawa kinga.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Theme images by rion819. Powered by Blogger.