Sunday, May 6, 2018

HAYA NDIYO MAGONJWA UNAYOPATA KUTOKANA NA HASIRA ZAKO

  Malunde       Sunday, May 6, 2018
Ni vigumu kuizuia hasira kama unaishi na watu. Lakini wataalamu wa afya wanasisitiza ni vyema kuzuia hasira kwani usipoizuia utakumbwa na maradhi mbalimbali ikiwamo ya moyo na kiharusi.

Hasira ni hisia zinazojitokeza dhidi ya kitu au mtu unayedhani amekufanyia jambo baya.

Vilevile hasira inaweza kuwa msaada kwa kumwezesha mtu kufikiri vizuri na kwa umakini. Hata hivyo, hasira si nzuri kiafya inapokutokea mara kwa mara na kushindwa kuidhibiti.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Sulenda Kuboja anakiri kwamba hasira kupita kiasi inaweza kusababisha magonjwa ya moyo na baadaye kifo.


Wataalamu wanasema hasira ikizidi inaweza kusababisha madhara kwenye mishipa ya fahamu na hivyo kuuweka moyo katika hatari kubwa ya kupata magonjwa.


Dk Kuboja anasema wapo watu ambao wakipata jambo linaloweza kuwasababishia hasira kali, mishipa ya fahamu huziba na mwisho kupata shambulio la moyo (heart attack).


“Wakati mwingine mishipa inaweza kujifunga unaposhtushwa na jambo ghafla. Hii inaweza kuwapata wale wenye matatizo ya moyo kwa muda mrefu au hata ambaye hajawahi kuwa na tatizo hilo,” anasema.


Pia, hasira husababisha kiharusi (stroke), ugonjwa unaoathiri ubongo na ufanyaji kazi wake. Wataalamu wa afya wanasema mara nyingi ugonjwa huo hujitokeza ghafla na Dk Kuboja anasisitiza kuwa ni rahisi ugonjwa huo kumpata mtu anayeshindwa kuhimili hasira.


“Unapopata hasira ghafla na ukashindwa kuzihimili, mishipa inaziba na ikishindwa kupitisha damu matokeo yake unaweza kupooza ghafla,” anasema Dk Kuboja.


Kwa watu wenye matatizo katika mishipa ya damu, hasira kupita kiasi zinaweza kuwaweka kwenye hatari ya kuongeza tatizo hilo mara sita zaidi. Pamoja na maradhi ya moyo na kiharusi, kadhalika hasira za muda mrefu zinapunguza kinga ya mwili.

Katika moja ya tafiti za Chuo Kikuu cha Harvard kilichopo Marekani, wanasayansi walibaini seli zinazoimarisha kinga mwilini hudhoofu kwa sababu ya hasira na hivyo kudhoofisha mfumo mzima wa mwili.

Wanasema hali hiyo inaufanya mwili kushambuliwa na magonjwa kwa urahisi hasa yale ya kuambukiza.

Pamoja na maradhi, lakini hasira za mara kwa mara zinamuweka mtu karibu na kifo.

Utafiti wa zaidi ya miaka 17 wa Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani ulibaini kuwa wenza (wanandoa) wanaobaki na hasira mioyoni muda mrefu wana maisha mafupi zaidi ya wanaozungumza pindi wanapokuwa nazo.

Mtaalamu wa saikolojia jijini Dar es Salaam, Josila Mageni anasema mtu mwenye hasira muda mwingi huwa na huzuni ambayo inamuweka kwenye hatari ya kupata magonjwa.

“Kama utakuwa na hasira mara kwa mara ipo hatari kubwa ya kupoteza furaha na muda mwingi utajikuta mwenye mawazo ukikumbuka mambo mabaya uliyotendewa,” anasema.

Dk Chris Peterson kutoka Dar es Salaam anasema mtu akiwa na hasira, hofu huanza kujijenga moyoni mwake.

“Huwa hajiamini, mwenye hofu na wasiwasi wakati wote na hapo huwa haijalishi jambo hilo analohofia ni zuri au baya,” anasema.

Huathiri mapafu

Sio tu matumizi ya sigara peke yake yanaweza kusababisha madhara kwenye mapafu, bali wanasayansi na watafiti mbalimbali wanasema hasira zinaweza kuathiri mapafu kuliko hata sigara.


Kundi la watafiti wa Chuo Kikuu cha Harvard walifanya utafiti kwa zaidi ya miaka minane kwa wanaume 670 ambapo walibaini kuwa hasira inaweza kusababisha viwango vya juu vya saratani ya mapafu.
Na Tumaini Msowoya, Mwananchi 

Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post