ZITTO KABWE: “WAZEE WA UJIJI SASA MKAE, TUMALIZE HAYA MAMBO YA KIPUUZI”

Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo amefunguka na kuonyesha kuchoshwa na baadhi ya mambo ambayo yanaendelea nchini na kuamua kuwaomba wazee wa Ujiji Kigoma wakae ili kuweza kumaliza mambo hayo anayodai ni ya kipuuzi.


Zitto Kabwe amesema hayo baada ya Idara ya Uhamiaji kumuhoji kuhusu uraia wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini Tanzania, Abdul Nondo jambo ambalo Zitto Kabwe anasema idara ya uhamiaji inatumika kisiasa dhidi ya mwanafunzi huyo.


"Sio kosa hata kidogo Abdul kuzaliwa Ujiji Kigoma. Imekuwa tabia ya Serikali kuwapa kesi za uraia watu wanaotoka mikoa ya magharibi hasa Kigoma. Suala la Nondo ni vita dhidi ya Watu wa Kigoma. Tutapambana. Tutampigania Abdul Nondo. Watanzania tusikubali upuuzi huu wa watu wa Uhamiaji kuwafanya raia wa mikoa kama Kigoma kuwa raia wa daraja B" alisema Zitto Kabwe


Aidha Zitto Kabwe alikwenda mbali na kusema kuwa mwanafunzi huyo ni mjukuu wa moja ya muasisi wa TANU ambaye pia alipigania uhuru wa Tanganyika


"Abdul Nondo Abdul Omar Mitumba, mjukuu wa Marehemu Mzee Omar Mitumba, mwasisi wa TANU na mpigania Uhuru wa Tanganyika leo anaitwa na maafisa Uhamiaji eti kuhojiwa uraia. Hao maofisa uhamiaji na aliyewatuma hawana 'credentials' ambazo Babu yake Nondo, Mwenyekiti wa TSNP anazo. Wazee wa Ujiji sasa mkae. Tumalize haya mambo ya kipuuzi" alisisitiza Zitto Kabwe


Mwanafunzi Abdul Nondo aliitwa jana idara ya uhamiaji kuhojiwa juu ya uraia wake na kujaza fomu hivyo anapaswa kufika tena ofisi za uhamiaji tarehe 20 mwezi huu kwa ajili ya kupeleka vyeti vya kuzaliwa yeye, baba na mama yake, na bibi na babu kwa pande zote mbili za wazazi wake

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527