RAIS MAGUFULI AWALILIA 12 WALIOFARIKI AJALI YA BASI LA CITY BOY

Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kufuatia ajali ya basi la kampuni ya City Boy iliyotokea jana Aprili 4, 2018 katika Kijiji cha Makomero Wilaya ya Igunga Mkoa wa Tabora na kusababisha vifo vya watu 12.


Ajali hiyo imetokea baada ya basi hilo lililokuwa limebeba abiria kutoka Karagwe Mkoa wa Kagera kuelekea Dar es Salaam kugongana uso kwa uso la lori lililokuwa likitokea Singida kuelekea Igunga.


Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Aprili 5, 2018 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema Rais Magufuli mbali na kutoa pole, amewataka viongozi wote wanaohusika na usimamizi wa usalama barabarani kutafakari kwanini ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika maeneo yaleyale na kutafuta ufumbuzi ili kuepusha madhara ya watu kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na kupoteza mali.


Rais amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote na amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahala pema peponi, majeruhi 46 wapone haraka.


“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 12 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani jana usiku katika wilaya ya Igunga mkoani Tabora, nawapa pole wafiwa wote, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msbia huu mkubwa,” amesema Rais Magufuli.


“Aidha, nalitaka Jeshi la Polisi, Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa na wilaya na mamlaka zote zinazohusika na usalama wa barabarani kujitathmini na kutafuta majawabu ya kwanini ajali za barabarani zinaendelea kutoka kwa kusababishwa na uzembe na uvunjaji wa sheria za barabarani.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527