MAMIA YA WANANCHI SYRIA WAJITOKEZA BARABARANI KUSHANGILIA USHINDI WAKIDAI SHAMBULIO LA MAREKANI LIMEFELI

Hisia mbalimbali zimejitokeza duniani ikiwa baadhi ya watu wanaunga mkono mashambulizi hayo na wengine kukosoa shambulizi hilo la anga lililofanywa mapema Jumamosi na majeshi ya Marekani, Ufaransa na Uingereza dhidi ya vituo vya serikali ya Syria.

Lakini hali ni tofauti kidogo Syria ambapo Mamia ya wananchi wa Syria wamejitokeza katika mji mkuu wa Damascus, Jumamosi hii wakiendesha magari huku honi zikilia, wakionyesha alama ya ushindi na kupeperusha bendera za Syria kwa kupinga mashambulizi ya kijeshi ya pamoja yaliyofanywa na nchi hizo tatu. Wengine walikuwa wakipiga makelele wakisema, "Sisi ni watu wako, Bashar."

Ndege za kivita za nchi za Ulaya na manuari za kijeshi zilishambulia kwa makombora vituo vitatu vya silaha za kemikali nchini Syria, shambulizi la awali ambalo linaweza kugeuka kuwa ni muendelezo wa kampeni ya kijeshi dhidi ya serikali ya Rais Bashar al- Assad na wanao muunga mkono.

Washirika wa Syria, ikiwemo Urusi wamesema kuwa shambulizi hilo la pamoja dhidi ya Syria limefeli. Wizara ya mambo ya nje imesema idadi kubwa ya makombora yaliyopigwa Syria yaliangamizwa na mfumo ya ulinzi wa serikali ya Syria.

Katika mkutano wa waandishi wa habari London Jumamosi, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema nia ya kuratibu mashambulizi haya sio kwa ajili ya “kuipindua serikali,” lakini ni “kupunguza na kuzuia” uwezo wa serikali ya Assad kutumia silaha za kemikali.

Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa haiwezi kusimama kando na “kutupia macho tu” wakati utawala wa Syria ukiendelea kutumia silaha za kemikali dhidi ya watu wake.

Huko Paris, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa tamko akisema, “ Hatuwezi kuvumilia kitendo cha kufanya matumizi ya silaha za nyuklia ni mwenendo wa kawaida,” akiongeza kuwa “ukweli wa taarifa na kuhusika kwa utawala wa Syria hauna mashaka.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anaunga mkono mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani, Ufaransa na Uingereza.

Amesema mashambulizi hayo ya angani yaliyofanywa yanapaswa kuwa onyo kwa utawala wa Syria kutoendelea kutumia silaha za sumu.

Wakati huohuo Serikali ya Iran imesema imesema kuwa Marekani, Ufaransa na Uingereza hazitaweza kupata manufaa yoyote kwa kuishambulia Syria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527