Tanzia : AGNES MASOGANGE AFARIKI DUNIA


Msanii anayepamba video za muziki (video queen) Agnes Gerald maarufu kama Masogange, amefariki dunia. 

Akithibitisha taarifa ya kifo hicho daktari Rama Ngoma wa hospitali ya Mama Ngoma, amesema Agnes amefariki dunia kwa tatizo la pneumonia na upungufu wa damu  leo jioni Ijumaa Aprili 20,2018, na alikuwa amelazwa hospitalini hapo kwa muda wa siku nne mpaka kifo kilipomkuta.

Kwa mujibu wa mwanasheria wake, Reuben Simwanzaamesema taarifa za kifo chake amezipata kupitia dada yake, saa chache zilizopita.

Kwa maelezo ya Simwanza, dada wa Masogange, Emma Gerald, ndiye aliyetoa taarifa hizo baada tu ya kutoka kumuona alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Mwanasheria huyo ambaye amedai yeye si msemaji zaidi, kuhusu nini chanzo cha kifo chake, alidai mara ya mwisho waliwasiliana naye siku mbili zilizopita kwa ujumbe wa simu ya mkononi.

“Unajua kuumwa kweli alikuwa anaumwa, kipindi cha kesi yake magonjwa ya hapa na pale ikiwamo presha, si unajua tena mambo ya kesi hayana mwenyewe, lakini baada ya kwisha tulikuwa tunataniana kwamba sasa nina imani utakuwa powa kwani kila kitu kipo sawa,”amesema Simwanza.

Hata hivyo amesema yupo njiani kuelekea hospitali kwa kuwa hakuweza kupata maelezo zaidi kutoka kwa dada yake huyo ambaye amemsikia akiwa analia tu.

Hivi karibuni, Masogange alihukumiwa kulipa faini ya Sh 1.5 milioni na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Alibainika kutumia dawa hizo kati ya Februari 7 na 14, 2017.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527