ACT WAMTAKA SPIKA WA BUNGE KUFANYA UCHUNGUZI MAALUM WA SH TRILIONI 1.5 ZILIZOPOTEA

Chama cha ACT-Wazalendo, kimemuandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai kikimuomba kufanya uchunguzi maalumu kuhusu kiasi cha Sh1.5 trilioni ambazo hazionekani kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema hayo jana Alhamisi Aprili 19, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ufafanuzi wa kauli na hoja zilizosemwa na CCM jana.


"Sasa hivi CCM wakithubutu kutochokoza ACT-Wazalendo, swali letu ni moja tu Sh 1.5 trilioni ziko wapi? Upinzani tuna wajibu wa kuhoji ili kuhakikisha Watanzania wanajua fedha zao zinakwenda wapi," amesema.


Shaibu amesema barua hiyo imeandikwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Jeremiah Maganja akimuomba Ndugai kutoa kibali maalumu kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ikutane na imuagize CAG kufanya ukaguzi kuhusu fedha ili zijulikane zilizokopelekwa.


"Matumaini yetu Spika Ndugai atazingatia maombi haya. Lengo letu Watanzania wajue ukweli kwa sababu kumekuwa na upotoshaji mkubwa ukiendelea kuhusu fedha hizi," amesema Shaibu.


Amesema chama hicho hakitarudi nyuma katika sakata hilo na kuwaomba Watanzania kuwaunga mkono hadi hatua ya mwisho ili kujua ziko wapi kwa sababu ni fedha nyingi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527