WATU WAWILI WAFARIKI, SITA HOI KWA KULA MZOGA WA NG'OMBE


Wakazi wawili wa Kijiji cha Ilonga Kata ya Mambwekoswe wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, wamekufa na wengine sita wamelazwa katika zahanati ya kijiji hicho wakipatiwa matibabu baada ya kula mzoga wa ng'ombe.

Taarifa kutoka kijijini hapo zimesema baada ya baadhi ya wakazi kula mzoga huo wa ng’ombe walianza kuhara na kutapika, hatua iliyozua taharuki kubwa kwa wananchi, wakidhani kuwa kumeibuka mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kijijini hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura amethibitisha kufa kwa watu hao wawili na wengine sita kulazwa katika zahanati ya kijiji hicho kwa matibabu kutokana na mkasa huo wa kula mzoga wa ng’ombe.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa wilaya alikanusha uvumi wa kuibuka kwa kipindupindu, kama ilivyozushwa kijijini hapo.

"Wakazi hao walikula mzoga wa ng'ombe ambaye alikufa mfupi baada ya kutibiwa na wataalamu wa mifugo.

“Si kuwa wameugua ugonjwa wa kipindupindu… hapana ni baada ya kula mzoga wa mnyama huyo," alisisitiza Binyura, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo.

Diwani wa Kata ya Mambwekoswe, Julius Kanowali alisema mkasa huo ulitokea juzi katika kijiji hicho cha Ilonga, ambapo watu wawili walikufa ghafla huku wengine sita wakiugua ghafla kuhara na kutapika.

IMEANDIKWA NA PETI SIYAME - HABARILEO KALAMBO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527