VIGOGO WA CHADEMA WAKIONGOZWA NA MBOWE WASHTAKIWA KWA UASI, MAANDAMANO YASIYO HALALI NA KUHAMASISHA CHUKI

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine watano wa chama hicho wamesomewa mashtaka manane katika Mahakama ya Kisutu ikiwemo kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwiline.


Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.


Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa la kwanza ni kufanya mkusanyiko ama maandamano yasiyo na uhalali.


Kwa pamoja wanadaiwa Februari 16, 2018 wakiwa barabara ya Mkwajuni kwa pamoja walikusanyika kwa lengo la kutekeleza mkusanyiko ili watu waliokuwepo eneo hilo waogope kuona maandamano ya kuvunja amani.


Kosa la pili ni kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali, ambapo linawakabili washtakiwa wote wakidaiwa kutenda kosa hilo Februari 16,2018 Barabara ya Kawawa maeneo ya Kinondoni Mkwajuni.


Kwa pamoja wanadaiwa wakiwa na watu wengine 12 ambao hawajafikishwa mahakamani wakiwa katika maandamano na mkusanyiko wa vurugu waligoma kutii amri ya kusambaratika na kuvunja mkusanyiko huo uliosababisha kifo cha Akwilana Akwiline na majeraha kwa maofisa wa Polisi.


Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa jingine ni kuhamasisha chuki kwa wanajamii isivyo halali, ambalo linamkabili Mbowe.


Inadaiwa Februari 16, 2018 akiwa viwanja vya Buibui Kinondoni DSM akihutubia wakazi wa maeneo hayo na DSM alitoa matamshi ambayo yangesababisha chuki kwa Jamii.


Pia kosa jingine linalomkabili Mbowe ni uchochezi na kusababisha chuki katika jamii, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16,2018.


Inadaiwa akiwa Uwanja wa Buibui Kinondoni DSM akihutubia wakazi wa DSM alitoa matamshi ambayo yangepelekea chuki katika Jamii.


Pia Mbowe anakabiliwa na kosa jingine la uchochezi wa uasi, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui Kinondoni DSM.


Inadaiwa akiwa na nia ya kupandikiza chuki na dharau dhidi ya uongozi uliopo madarakani alitoa maneno ambayo ni wazi yangesababisha uasi.


Pia kosa jingine linalomkabili Mbowe ni uchochezi wa uasi, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui, Kinondoni DSM.


Inadaiwa akihutubia mkutano wa hadhara alitoa matamshi ambayo yangepandikiza chuki na dharau kwa wananchi wa Tanzania dhidi ya uongozi uliopo madarakani.


Kosa la saba linamkabili Mbowe ambalo ni ushawishi wa utendekaji wa kosa la jinai, ambalo amelitenda Februari 16, 2018 maeneo ya Buibui Kinondoni DSM.


Inadaiwa Mbowe akiwa amejumuika na watu wengine aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo na DSM kutenda kosa.


Katika kosa la 8, Wakili Nchimbi amedai linamkabili Msigwa ambalo ni kushawishi raia kutenda kosa la jinai.


Msigwa anadaiwa ametenda kosa hilo Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui Kinondoni DSM, ambapo aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo na DSM kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.


Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana ambapo Wakili Nchimbi amedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.


Hata hivyo, Wakili Nchimbi aliwasilisha maombi kwa mahakama hiyo ili washtakiwa wanyimwe dhamana kwa sababu ya usalama wa umma wa Watanzania.


Na Tausi Ally, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527