Picha: TGNP MTANDAO YAENDESHA WARSHA KWA WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA...YATAKA WAZAME VIJIJINI


TGNP Mtandao imeendesha warsha kwa waandishi wa habari mkoani Shinyanga kwa lengo la kujadili namna ya kusaidia kupaza sauti za wanyonge hususani wanaoishi maeneo ya vijijini. 

Warsha hiyo ya siku moja imefanyika leo Ijumaa Machi 23,2018 katika ukumbi wa Diamond Fields Hotel mjini Shinyanga.

 Akizungumza wakati wa warsha hiyo,Mragbishi kutoka TGNP Mtandao Annagrace Rwehumbiza aliwataka waandishi wa habari mkoani Shinyanga kujikita zaidi kuandika habari za uchunguzi kwa kuibua matatizo ndani ya jamii, ambayo yamekuwa yakifichika  jambo ambalo litawasaidia wananchi kutatulia kero ambazo zimekuwa zikiwakabili sababu ya kukosa sehemu pa kuzisemea. 

Alisema waandishi wa habari wana msaada mkubwa ndani ya jamii kwa kupaza sauti za wanyonge kupitia kalamu zao kwa kuibua matatizo ambayo yamekuwa yakiwakabili wananchi, na hasa kwa kuandika habari za uchunguzi ili jamii ipate kutatuliwa kero zao. 

“Naombeni waandishi wa habari mkoani Shinyanga mjikite zaidi kuandika habari za uchunguzi kwa kuibua matatizo ambayo yamekuwa yakijificha ndani ya jamii, hususani kwa wale wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini, ambao wamekuwa wakikosa wa kuwapazia sauti na kuendelea kuishi maisha ya shida,”alisema Rwehumbiza. 

Aidha alitolea mfano Kata ya Bunambiu iliyopo wilayani Kishapu, ambapo wananchi wake wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la mauaji kwa kukatwa mapanga hususani pale wanapodai haki zao hasa wanawake, lakini suala hilo wamekuwa wakikaa nalo kimya na kukosa wa kuwa semea huku wakiendelea kuuawa. 

Naye mmoja wa wananchi wa kata hiyo ya Bunambiu Everada Mayuma, alisema wananchi wamekuwa waoga kutoa taarifa za matukio mbalimbali kwa kuogopa kukatwa mapanga, na hivyo kuendelea kuishi maisha ya shida sababu ya vitisho hivyo. 

Nao baadhi ya waandishi wa habari Shabani Alley kutoka kituo cha Matangazo Star tv na Kadama Malunde  ,mwandishi wa Malunde 1 Blog, waliwatupia lawama wananchi hususani wa maeneo hayo ya vijijini, ambapo wamekuwa waoga kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kwa kushindwa kuzungumza matatizo yanayowakabili.

Walisema kwa nyakati tofauti kuwa waandishi wa habari hawezi kuchunguza habari bila ya kupewa taarifa (tipu) juu ya tatizo linalowakabili wananchi, pamoja na kutozungumza na wahusika waliofanyiwa matukio hayo ya ukatili ama ndugu, ambapo wananchi hao huwa hawapo tayari kuzungumza na kuwakimbia waandishi.

Naye mwandishi wa habari Stephen Kidoyayi wa Gazeti la Tanzanite aliwataka wananchi kuachana na tabia za uoga pale wanapotaka kusemewa matatizo yanayowakabili kupitia vyombo vya habari, bali wawe karibu na vyombo hivyo ambavyo ndiyo msaada mkubwa kwao.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Muraghbishi kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Annagrace Rwehumbiza akizungumza na waandishi wa habari mkoani Shinyanga leo katika ukumbi wa Diamond Fields Hotel Mjini Shinyanga 
Annagrace Rwehumbiza akizungumza ukumbini
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga (SPC)  Kadama Malunde ambaye pia ni Mmiliki wa mtandao wa Malunde 1 Blog akichangia mada kwenye warsha hiyo ya siku moja kwa  waandishi wa habari na (TGNP) Mtandao, Kuwa tatizo la wananchi wa maeneo ya Vijijini hua waoga kusema matatizo ambayo hua yanawakabili na hata kama wakihojiwa na vyombo vya habari hua hawapo tayari kuzungumza na kuwataka wavunje ukimya huo iliwapate kusemewa matatizo yao na kupatiwa ufumbuzi.
Makamu mwenyeki wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mwandishi wa habari Star tv Shabani Alley akizungumza kwenye warsha hiyo.
Muraghbishi kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Annagrace Rwehumbiza akielezea changamoto ambazo amekutana nazo kwenye kata ya Bunambiu wilayani Kishapu wakati akifanya kazi ya kuibua matatizo yanayowakabili kuwa ni unyanyasaji wa kijinsia, mfumo kandamizi hasa kwenye suala kilimo ambapo wanawake ndiyo huenda mashambani huku waume zao wakikesha kucheza bao,kunywa kahawa, uhaba wa maji, lugha chafu kwa wauguzi wa afya,miundombinu mibovu ya barabara, ukosefu wa mabweni kwa shule ya sekondari Bunambiu, wanawake kuuawa kwa kukatwa mapanga, pamoja na ubabe wa viongozi na kutotatua kero za wananchi.
Mwandishi wa habari Suleiman Abeid wa Tv Imaan akizungumza ukumbini
Wanakikundi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka kata ya Bunambiu wakiwa kwenye warsha ya (TGNP) Mtandao na Waandishi wa habari mkoani Shinyanga.
Waandishi wa habari wakiwa ukumbini
Mwandishi wa habari Josephine Charles kutoka Radio Faraja akiwa ukumbini
Mwandishi wa habari wa ITV Frank Mshana akizungumza kwenye warsha hiyo amewataka pia wananchi kuacha tabia ya uoga kusema matatizo yanayowakabili bali wawe wawazi ili yapate kutatuliwa na kuishi kwa amani na siyo kukaa kimya.
Katibu Mtendaji klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni mwandishi wa habari wa AZAM TV Stephen Wang'anyi akichangia mada kwenye warsha hiyo.
Waandishi wa habari wakiwa kwenye warsha hiyo
Mwandishi wa habari wa Daily News Suleiman Shaghata akichangia mada kwenye warsha hiyo.
Mratibu wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga (SPC) Henry Estomine akizungumza kwenye warsha hiyo, ambapo amewataka wana kikundi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka Kata ya Bunambiu wilayani Kishapu ambao wamepewa mafunzo na (TGNP) kuhakikishiwa usalama wao sababu pale matatizo ama maovu ambayo yatakuwa yakiibuliwa na waandishi wa habari wao ndiyo watanyooshewa vidole na maisha yao kuwa hatarini kutokana na maelezo kuwa mtu akionekana kiherehere huwa ana pewa vitisho ama kukatwa mapanga.
Naye mwandishi wa habari Stephen Kidoyayi wa Gazeti laTanzanite akizungumza katika warsha hiyo ambapo amewataka wananchi kuachana na tabia za uoga pale wanapotaka kusemewa matatizo yanayo wakabili kupitia vyombo vya habari, bali wawe karibu na vyombo vya habari ambazo ndio msaada mkubwa kwao.

Waandishi wa habari wakiwa kwenye warsha. 
Mwandishi wa habari Moshi Ndugulile wa Radio faraja (wa kwanza mkono wa Kushoto) akiwa na Mwandishi wa habari wa ITV Frank Mshana kwenye warsha hiyo.
Mwandishi wa habari wa ITV Frank Mshana (Kushoto) akiwa na Mwandishi wa Nipashe na Shinyanga News Blog Marco Maduhu.
Mwandishi wa habari wa Star Tv Shabani Alley akichangia Mada kwenye Warsha hiyo, huku wa kwanza kulia ni Mwandishi wa Radio Faraja Isack Edward (kushoto) ni Yohana Emmanuel wa Divine FM.
Wana kikundi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka kata ya Bunambiu wilayani Kishapu wakiwa kwenye warsha ya (TGNP) Mtandao na Waandishi wa habari mkoani Shinyanga.
Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani Shinyanga( SPC)Kadama  Malunde  akizungumza jambo wakati wa kufunga warsha hiyo ya siku moja kati ya (TGNP) Mtandao na waandishi wa habari mkoani Shinyanga iliyokuwa na lengo la kukumbushana na kuwekana sawa namna ya kusaidia wananchi wa maeneo ya vijijini kuwasemea matatizo yanayowakabili kwa kutumia kalamu zao na kuzitoa taarifa hizo kupitia media wanazofanyia kazi.

Picha na Marco Maduhu & Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527